Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Wilayani Same Watakiwa Kufanya Kazi kwa Uwazi na Kuzingatia Sheria
WENYEVITI WA VIJIJI NA VITONGOJI WILAYANI SAME WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UWAZI NA KUZINGATIA SHERIA.
Same, Kilimanjaro.
Wenyeviti wa vijiji na vitongoji wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo. Aidha, wamehimizwa kusimamia kwa uwazi mapato na matumizi ya vijiji vyao, kutoa taarifa za miradi inayotekelezwa, na kuhakikisha wanashughulikia kero na malalamiko ya wananchi kwa ufanisi ili kuimarisha utawala bora.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ametoa wito huo wakati wa mafunzo maalumu kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji, yanayofanyika wilayani humo kwa muda wa siku mbili. Mafunzo haya yanalenga kuwaongezea viongozi hao uelewa na uwezo, kujua majukumu yao ya utendaji na ya msingi kama wenyeviti wa vijiji na vitongoji ili kuongoza kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Kasilda amewataka wenyeviti hao pia kuhakikisha usalama wa mipaka ya maeneo yao kwa kuzuia uhamiaji holela wa wananchi wanaoingia bila utaratibu kwa lengo la kuendeleza shughuli zao ilhali hawana maeneo rasmi. Amebainisha kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi, pamoja na mvutano baina ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya maeneo.
"Ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa mnatekeleza majukumu yenu kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo. Miradi yote lazima iendeshwe kwa uwazi, mapato na matumizi yasomwe kwa wananchi, na kero zao zitatuliwe kwa wakati. Pia, tunapaswa kulinda mipaka yetu ili kuepusha migogoro inayoweza kuzuka kutokana na uhamiaji holela," amesisitiza Mhe. Kasilda.
Aidha, amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kushirikiana, kufuata ngazi za Uongozi katika malalamiko pamoja na kero, kuwa suluhisho la changamoto za wananchi, na kutoonyesha upendeleo katika utendaji wao.
Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Muhsin Danga, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, amesema mafunzo hayo yanajikita katika mada za uongozi na utawala bora, muundo na sheria za uendeshaji wa Serikali za Mitaa, usimamizi wa fedha na ardhi, pamoja na uibuaji na upangaji wa mipango endelevu.
Baadhi ya wenyeviti hao wameeleza kuwa kuna baadhi ya mambo yalikuwa yakiwatatiza kutokana na wengi wao kuwa wapya katika nagasi za uongozi, hivyo wameshukuru kwa mafunzo hayo na kuahidi kwenda kufanya kazi kulingana na maelekezo ya mafunzo hayo.
Mafunzo haya yanawahusisha wenyeviti 100 wa vijiji na wenyeviti 503 wa vitongoji, na yanatarajiwa kuboresha utendaji wao katika kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa. Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Comments
Post a Comment