MKUU WA WILAYA YA SAME AWATAKA WASIMAMIZI WA MIRADI KUTOA USHIRIKIANO KWA MAAFISA WA SERIKALI.
MKUU WA WILAYA YA SAME AWATAKA WASIMAMIZI WA MIRADI KUTOA USHIRIKIANO KWA MAAFISA WA SERIKALI.
Same, Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewataka wasimamizi wa miradi inayoendelea kujengwa ndani ya wilaya hiyo kushirikiana na maafisa wa serikali wanapofanya ziara za ukaguzi. Amesisitiza kuwa ziara hizo zina lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha, na kasi inayotakiwa ili kuepusha ubadhilifu na ujenzi wa majengo yasiyo na viwango stahiki.
Mhe. Kasilda alitoa kauli hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Hedaru, katika ziara hiyo aliambatana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Same ambapo Alibainisha kuwa maafisa wa serikali na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya wanapokagua miradi, wanakuwa na nia njema ya kushauri na kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.
![]() |
Mkuu wa wilaya ya Same Mhe Kasilda Mgeni akijaza udongo kwenye ndoo kitendo kinachoonesha ushiriki katika ujenzi wa mradi wa shule hiyo. |
"Katika miradi yote inayoendelea wilayani hapa, nawasihi wasimamizi wa miradi kutoa ushirikiano kwa maafisa wa serikali. Pale watakapoona changamoto, watawashauri ili kuhakikisha mradi unakuwa bora na unakidhi viwango vinavyotakiwa," alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka za miradi ili viongozi wanapofanya ukaguzi waweze kuona uwiano kati ya fedha zilizotolewa na kazi inayoonekana. Pia alihimiza ukaguzi wa vifaa vinavyopokelewa ili kuhakikisha ubora wake katika utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Same, Bw. Daimon Mwakababu, aliwataka wasimamizi wa miradi, viongozi wa siasa, na serikali kutoingilia majukumu ya TAKUKURU. Alisisitiza kuwa taasisi hiyo haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa miradi au kujihusisha na vitendo vya ubadhilifu.
![]() |
Katibu Tawala wa Wilaya ya Same Bi. Upendo Wela na Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Same Bw. Daimon Mwakababu wakishiriki shughuli za ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Kata ya Hedaru. |
"Ili fedha za serikali zitumike ipasavyo, nawasihi watumishi wa umma wanaosimamia miradi pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi kutoingilia kazi za TAKUKURU. Tuacheni tufanye kazi kama alivyoagiza Mhe. Rais. Hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayejihusisha na uhalifu wa aina yoyote," alisema Bw. Mwakababu.
Awali, akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mwalimu wa Shule ya Mkombozi, Upendo Nathaniel, alisema kuwa kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mkombozi na kupunguza umbali wanaotembea kufuata elimu.
Zaidi ya shilingi milioni 584 zinatumika katika ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Kata ya Hedaru, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 248 zimeshatumika. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 31, mwaka huu.
Comments
Post a Comment