WAZIRI KOMBO ATOA WITO WA USHIRIKIANO WA KWELI KATI YA AFRIKA NA NCHI ZA NORDIC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amezihimiza nchi za Afrika na Nordic kuhakikisha kuwa ushirikiano wao unazaa matokeo halisi kwa wananchi, akisisitiza kuwa mashirikiano hayo hayapaswi kubaki kwenye makaratasi tu bali yawe na athari inayopimika.
Akizungumza katika Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika Victoria Falls, Balozi Kombo alisema mkutano huo ni jukwaa mahsusi la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijamii huku ukihamasisha biashara, uwekezaji, teknolojia, na nishati safi.
“Ushirikiano huu haupaswi kubaki wa kinadharia. Ni lazima tuyageuze mazungumzo kuwa hatua za vitendo zitakazoboresha maisha ya watu wetu moja kwa moja,” alisema, huku akieleza utayari wa Tanzania kushirikiana na nchi za Nordic katika miradi ya kimkakati yenye matokeo ya haraka na yanayoonekana.
Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi Suzan Kaganda, aliwahimiza washiriki kutumia fursa ya mkutano huo kuendeleza diplomasia ya kiuchumi katika sekta mbalimbali kama vile biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, elimu, na usalama
Naye Balozi wa Tanzania nchini Uswidi, Mobhare Matinyi, alibainisha fursa kubwa ya biashara na uwekezaji iliyopo Tanzania, akisema nchi hiyo ni lango muhimu kwa ushirikiano kati ya mataifa ya Nordic na Afrika.
Mkurugenzi Mkaimu wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Seifu Kamtunda, alisema kwamba mijadala ya mkutano huo itajikita katika masuala muhimu ya kuimarisha mahusiano kati ya Afrika na nchi za Nordic.
Aidha, kongamano la kibiashara litawakutanisha wajasiriamali, wadau wa sekta binafsi, wavumbuzi vijana, na taasisi za elimu ya juu kwa lengo la kuchunguza fursa za ushirikiano.
Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 3, 2025, umebeba kaulimbiu isemayo: “Ubunifu kwa Matokeo: Kutumia Teknolojia na Ushirikiano kwa Jamii za Baadaye Zilizo Tayari.”
Taaisisi za Tanzania kama TIC, ZIPA, TCCIA pamoja na idara mbalimbali ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje zinashiriki kikamilifu ili kuonyesha vipaumbele vya taifa na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia na nchi za Nordic.
Comments
Post a Comment