MABADILIKO YA MTINDO WA MAISHA YASISITIZWA KUPITIA VIONGOZI WA DINI NA WA KIMILA KUKABILI MARADHI YATOKANAYO NA LISHE

 

MABADILIKO YA MTINDO WA MAISHA YASISITIZWA KUPITIA VIONGOZI WA DINI NA WA KIMILA KUKABILI MARADHI YATOKANAYO NA LISHE.

Na Christina Thomas.

Same, Kilimanjaro. 

Kulingana na takwimu za Lishe Kitaifa kwa mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 30 (watoto 3 kati ya 10) walio na umri chini ya miaka mitano wamedumaa, asilimia 12 (mtoto mmoja kati ya 10) walio na umri chini ya miaka mitano wana uzito pungufu hali inayoweza kuwasababishia magonjwa ya mara kwa mara, athari mbaya za ukuaji kimwili, kiakili na kisaikolojia.

Pia takwimu za mwaka 2022 zinaonesha asilimia 42 ya hali ya lishe kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (miaka 15-49) wana upungufu wa damu, mwanamke 1 kati ya 10 ana uzito pungufu (amekonda), na takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuongezeka kwa idadi ya wanawake wenye tatizo la unene uliopitiliza hadi kufikia asilimia 36.

Kulingana na hali ya Takwimu hizo, Serikali ya Wilaya ya Same imeamua kuwekeza nguvu kwa Viongozi wa Dini mbalimbali pamoja na viongozi wa Kimila ndani ya Wilaya ya Same kutumia majukwaa yao yanayowakutanisha na jamii ikiwemo mikusanyiko ya ibada kuelimisha na kuhamasisha juu ya masuala ya Afya, Lishe na mtindo bora wa maisha mara kwa mara ili kutatua kupunguza matokeo mabaya ya lishe duni.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wa Afua za Afya na Lishe kwa Viongozi wa Dini ndani ya Wilaya ya Same, Katibu Tawala Msaidizi wa Wilaya ya Same Ndg. Sixbert Sylvester ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni amesema uzingatiaji wa lishe unasaidia kuongeza ubora wa maisha, kuimarisha kinga ya mwili, Afya ya akili pamoja na kupunguza gharama za matibabu ya magonjwa yanayotokana na lishe duni.

“Serikali ina imani kubwa na ninyi, tutakapounganisha nguvu na kuendelea kutumia fursa ya majukwaa yao kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya maswala ya afya na lishe tutaweza kufikia adhma ya kuboresha afya na ustawi wa jamii kwa ujumla, hivyo, wito wa serikali kwenu pia endeleeni kuhamasisha jamii kuhusu utoaji wa chakula shuleni, upandaji wa miti ikiwemo ya matunda maeneo ya makazi, ufugaji wa kuku pamoja na kilimo cha Mbogamboga”. Amesema Ndg. Sixbert Sylvester.

Akielezea lengo la mafunzo hayo, Afisa Afya wa Wilaya ya Same Bi. Yuster Malisa amesema kuwa viongozi wa Dini na wa Kimila wana idadi kubwa ya watu wanaokutana nao mara kwa mara, ambapo baadhi ya mada ni pamoja na mafunzo ya hali ya lishe, mlo kamili na makundi ya vyakula, mtindo bora wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza, afua za afya ya uzazi na mtoto pamoja na magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wake Afisa lishe wa wilaya ya Same Bi. Jackline Kilenga amesema kuwa jamii bado inakabiliwa na changamoto ya Lishe duni kwa makundi na rika zote ikiwemo changamoto ya udumavu kwa watoto, uzito uliozidi huku akieleza kuwa viongozi wa dini na wa kimila watawasaidia kwa asilimia kubwa katika kuelimisha jamii.

Ukosefu wa lishe bora huathiri afya ya binadamu kwa njia mbalimbali, kuanzia matatizo ya kiafya hadi kudhoofisha mifumo muhimu ya mwili. Moja ya madhara makubwa ni udumavu, hali inayosababisha watoto kukua kwa kuchelewa na kuwa na kinga dhaifu dhidi ya magonjwa. Udumavu unaweza pia kuathiri uwezo wa kujifunza na hatimaye kupunguza tija katika maisha ya baadaye.

Aidha, lishe duni huweza kusababisha magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu, na magonjwa ya moyo. Ulaji usiofaa wa virutubishi muhimu kama protini, madini, na vitamini huathiri mifumo ya mwili, na kusababisha udhaifu wa misuli na matatizo ya viungo. Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa watoto, wanawake wajawazito, na wazee ambao miili yao inahitaji lishe bora kwa ukuaji na uimara wa afya.

Zaidi ya hayo, ukosefu wa lishe bora huathiri afya ya akili kwa kusababisha mfadhaiko, uchovu wa mara kwa mara, na kushuka kwa uwezo wa kufikiria. Upungufu wa virutubishi kama chuma na vitamini B huweza kusababisha anemia na matatizo ya utendaji wa ubongo. Hii inadhihirisha kuwa lishe bora si tu suala la afya ya kimwili, bali linaathiri pia ustawi wa akili na uwezo wa mtu kufanya kazi kwa ufanisi.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO