KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA HIFADHI YA MAKUYUNI

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA HIFADHI YA MAKUYUNI

Na. Mwandishi Wetu. 

Arusha.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), katika Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni almaarufu kama "Makuyuni Wildlife Park" iliyopo Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha.

Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo, tarehe 13 Machi, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) alisema Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 30 iliyogharimu shillingi milioni 256 pamoja na bwawa lenye uwezo wa kubeba maji lita milioni 52 lililogharimu shilingi milioni 125.

"Kwanza tuipongeze Serikali kwa hatua ya kuchukua eneo hili muhimu na kuwakabidhi TAWA, pia niwapongeze TAWA kwa ukarabati na ufunguaji wa barabara wa hifadhi hii pamoja na ile ya ujenzi wa bwawa, kama Kamati tumeiona kazi TAWA mliyoifanya katika eneo hili ni kazi nzuri, tunawapongezeni sana na tumeridhika na kazi hii", alisema Mhe. Mnzava.

Aidha, Mhe. Mnzava alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya kitalii iendelee kufanyika katika maeneo mengine ya hifadhi ili kuhakikisha kuwa watalii wanapokuja katika hifadhi zetu hawapati changamoto zozote.

Kwa upande wake, Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb), alisema kuwa ujenzi huu wa barabara umetumia gharama nafuu kwa kuzingatia kuwa mitambo iliyotumika kwenye ujenzi wa miundombinu hii ilinunuliwa na Serikali kupitia Mpango wa Ustawi wa Jamii na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Kadhalika, Mhe. Chana aliwahakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa ushauri na maelekezo yote waliyoyatoa kwa Wizara kwa kupitia TAWA yatatekelezwa kikamilifu.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko, aliishukuru Kamati kwa kufanya ziara katika Hifadhi ya Makuyuni na alisema kuwa Menejimenti yake imepanga kuifanya Hifadhi ya Makuyuni kuwa kitovu cha utalii katika jiji la Arusha, hususani kwa watalii wa ndani. 

Sambamba na hilo, Semfuko aliongeza kuwa TAWA itaendelea kuongeza ubunifu kwenye utendaji kazi wake kama ambavyo imefanya kwenye mapinduzi ya ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada wa kielektroniki.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO