WITO WATOLEWA KUWACHUKULIA HATUA ZA KIUTUMISHI MAAFISA UTUMISHI WAZEMBE WANAOWAKOSESHA HAKI ZA MSINGI WALIMU.
WITO WATOLEWA KUWACHUKULIA HATUA ZA KIUTUMISHI MAAFISA UTUMISHI WAZEMBE WANAOWAKOSESHA HAKI ZA MSINGI WALIMU.
Na Christina Thomas
Same, Kilimanjaro.
Imeelezwa kuwa Watumishi wa kada ya Ualimu wakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kucheleweshwa kupandishwa madaraja, kubadilishwa kwa miundo baada ya kujiendeleza, malimbikizo ya mishahara, madai ya muda mrefu ya stahiki za uhamisho, taarifa chafu kwenye mfumo pamoja na madai ya kustaafu ambapo baadhi ya changamoto hizo zimetajwa kusababishwa na baadhi ya maafisa utumishi wazembe wanaowakosesha haki za msingi watumishi wa Umma wakiwemo walimu.
Kutokana na hilo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesisitiza kuwa ni vyema mamlaka husika kuwachukulia hatua baadhi ya maafisa Utumishi ambao watabainika kufanya uzembe kwa makusudi kuwakosesha haki za msingi watumishi wa Umma wakiwemo walimu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.
Akizungumza katika kliniki ya kutatua changamoto za walimu (Samia Teacher's Mobile Clinic) iliyowakutanisha walimu kutoka wilaya ya Mwanga na Same, katika ukumbi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni ameeleza kuwa changamoto nyingi wanazokutana nazo walimu zinaathiri utendaji wao wa kazi, hivyo kupunguza ubunifu na ufanisi.
"Walimu wanapokumbwa na changamoto nyingi, utendaji wao lazima ushuke hakutakuwa na ubunifu, na hali hii inaathiri ubora wa elimu. Changamoto hizi zinatokana na baadhi ya maafisa utumishi wazembe, wanaowakosesha haki za msingi watumishi wa Umma kwakiwemo walimu kwa makusudi. Nakuomba sana, Mkurugenzi wa Utumishi, maafisa hawa wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine," amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na timu inayojumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakishirikiana na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ili kupita mikoa mbalimbali nchini kusikiliza na kutatua changamoto za walimu ambapo amepongeza njia hii akisema kuwa ni bora na salama zaidi, kwani inarahisisha namna ya uwasilishaji na utatuzi wa changamoto zinazowakabili walimu kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Suleiman Ikomba amesema kuwa wapo watu waliokuwa hawana nia njema na walimu, waliofikiri kutumia njia ya 'kupiga kelele' kudai madai yao kwa kupita barabarani njia ambayo inahatarisha utatuzi wa changamoto zao.
"Kuna watu wangefikiri tudai madai yetu kwa kupiga kelele na kupita barabarani, hapana, kumbe kuna serikali sikivu na tumeipata, tumeongea nayo na imetuelewa leo tupo hapa na uzuri huu umekuja katika njia ambayo bado tumebaki vizuri na tunaona matatizo yetu yanaenda kutatuliwa" amesema Mwalimu. Ikomba.
Comments
Post a Comment