WANANCHI KILIMANJARO WAISHUKURU SERIKALI KUPELEKA MADAKTARI BINGWA WA MACHO.
WALIOSUMBULIWA NA MACHO KILIMANJARO WAISHUKURU SERIKALI KUPELEKA MADAKTARI BINGWA WA MACHO.
Na Mwandishi Wetu.
Wananchi waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya kuona mkoani Kilimanjaro wameishukuru
Serikali kwa kuwaletea madaktari bingwa wa macho kutoka nchini Marekani na
kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa hayo na ushauri wa kitaalam, tiba kwa upasuaji
wa mtoto wa jicho na kuweza kuona upya.
Madaktari
hao ambao wamepiga kambi ya wiki mbili katika hospitali ya Wilaya ya Same ambapo
watu zaidi ya elfu mbili (2000) wamefanyiwa uchunguzi huku wagonjwa zaidi ya
tisini (90) wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hospitalini hapo mmoja kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Bw. Idd Mlaki, Mkazi wa Kileo wilayani Mwanga alieleza kuwa kwa muda wa miezi sita alikuwa haoni tatizo ambalo lilianza ghafla ambapo kwa sasa mara baada ya kupata huduma hiyo hali yake ya kuona imerejea tena.
“Macho
yangu yalikufa ghafla nikawa sioni mbele wala nyuma, na ikawa mtu
anaponisemesha nilikuwa nakasirika maana sioni na nimehangaika hospitali
mbalimbali bila mafanikio lakini leo
nimekuja hapa Same na kukutana na wataalam wakanichuna macho yangu mpaka
nikaona tena” alisema Bw. Mlaki.
Mlaki
alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuonyesha upendo mkubwa
kwa Watanzania na kuendelea kumwomba aendelee kuwasaidia watu wenye uhitaji wa
msaada mbalimbali.
Naye
Mwanaidi Mdoe mkazi wa Kisiwani wilayani Samwe, alisema kuwa, yeye alikuwa na
tatizo la kutokuona jicho moja kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo hakupata
ufumbuzi lakini kuja kwa wataalam hao imekuwa neema kwake ambapo kwa sasa
ameweza kuona tena.
Akizungumzia
kuhusu huduma hiyo Mratibu wa macho ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya
Same, Theodora Mwacha alisema kuwa, huduma hiyo ya macho inatolewa na madaktari
kutoka Marekani ambapo wanafanya huduma za uchunguzi wa macho na kutoa dawa kwa
wagonjwa wenye uhitaji pamoja na miwani.
Theodora alisema kuwa, huduma kubwa wanayoitoa ni huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho ambapo imekuwa faraja kubwa kwa wazee ambao wao ndio wameonekana kukumbwa kwa kiasi kikubwa na tatizo hilo.
“Huduma
hii inatolewa bure na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro
wamefika kuhudumia ambapo zoezi hili linatarajiwa kukamilika Machi 15 mwaka huu
na mpaka sasa tumeshawahudumia wagonjwa zaidi ya 2000 huku wagonjwa zaidi ya 90
wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho” alisema Theodora.
Mwisho..
Comments
Post a Comment