WATAKAOBAINIKA KUHUSIKA KUCHOMA MOTO BWENI LA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MAKANYA KUCHUKULIWA HATUA.
WATAKAOBAINIKA KUHUSIKA KUCHOMA MOTO BWENI LA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MAKANYA KUCHUKULIWA HATUA.
Na Christina Thomas.
Same, Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kuwafukuza shule wale wote watakaobainika kuhusika na tukio la moto lililoteketeza jengo la bweni la wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Makanya. Moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, kuteketeza vifaa vya wanafunzi kama magodoro, nguo, madaftari na mali nyinginezo.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka kwa wadau wa maendeleo wilayani Same, Mhe. Kasilda Mgeni alieleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo uko katika hatua za mwisho na kuahidi kuwa wahusika wote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Pia, mkuu wa Wilaya amewashukuru wadau wote waliotoa michango yao ya hali na mali kwa ajili ya wahanga wa tukio hilo wakiwemo Mwembe Logistics, Benki ya NMB, Madhehebu ya Dini pamoja na wadau wengine ambapo michango hiyo inajumuisha magodoro, matranka, vyandarua, fedha zaidi ya milioni nne, madawati, pamoja na vifaa vingine muhimu kwa matumizi ya wanafunzi waliopata hasara kutokana na janga hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Ndg. Abdallah Mnyambo, aliwataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya shule, akibainisha kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha sekta ya elimu, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi wa mali hizo za umma.
Akizungumza kwa niaba ya wadau waliotoa msaada huo, Afisa Masoko na Uhusiano wa Kampuni ya Mwembe Logistics, Bi. Janeth Mtui, alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya kuwatia faraja wanafunzi hao kutokana na madhara waliyoyapata. Alisisitiza kuwa kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii katika majanga mbalimbali.
Aidha, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mwalimu Neema Lemunge, alieleza athari zilizobainika kutokana na moto huo, akisema kuwa wanafunzi 14 walipata mshtuko na kupatiwa huduma za matibabu, ambapo hali zao kwa sasa zimeimarika. Pia, alieleza kuwa magodoro 22, nguo, madaftari, vitabu, na matranka viliteketea kwa moto, huku thamani ya hasara hiyo ikikadiriwa kuwa zaidi ya milioni tano.
Mmoja wa wanafunzi waliothirika na tukio hilo aliishukuru serikali pamoja na wadau kwa msaada waliotoa, huku akiahidi kuwa wanafunzi watahakikisha wanatunza miundombinu ya shule ili kuepuka majanga kama hayo siku zijazo.
Comments
Post a Comment