RAIS SAMIA AZINDUA MRADI WA MAJI WA SAME-MWANGA-KOROGWE.
RAIS SAMIA AZINDUA MRADI WA MAJI WA SAME-MWANGA-KOROGWE.
Mwanga, Machi 9, 2025
Na Musa Mathias.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe katika hafla iliyofanyika wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Mradi huu mkubwa, ambao umekuwa ukisuasua kwa takriban miaka 20, sasa umekamilika na utawezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa wilaya za Same, Mwanga, na Korogwe.
Katika hotuba yake, Rais Samia mara baada ya kuzindua mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe, akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro alielezea changamoto zilizokumba utekelezaji wa mradi huu, ikiwemo kusukumana, kusutana, na hata kushitakiana na makandarasi.
“Leo tunashuhudia matunda ya uvumilivu na juhudi za pamoja. Mradi huu ulianza kwa ahadi tangu enzi za watanyulizibwangu, lakini sasa, miaka kadhaa baadaye, tumeweza kuutekeleza na wananchi wameanza kunufaika,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa ipasavyo. Mabadiliko haya ni ushahidi wa juhudi na dhamira ya dhati ya serikali yetu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huu ni ishara ya jinsi serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza miradi kwa vitendo.
“Tuliahidi kuondoa kero ya maji kwa wananchi wa Same, Mwanga, na Korogwe, na leo tunaona ahadi ikitimia. Hatutarudi nyuma katika dhamira yetu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama,” alisema Waziri Aweso.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, aliishukuru serikali kwa dhamira yake ya dhati katika kutatua changamoto za maji katika mkoa huo. “Kwa miaka mingi wananchi wa Kilimanjaro wamekuwa wakihangaika kupata maji, lakini sasa historia inabadilika,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Mradi huu unachukua maji kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu na utahudumia zaidi ya wakazi katika wilaya za Same, Mwanga, na Korogwe. Awamu ya kwanza ya mradi huu imekamilika kwa gharama ya Shilingi bilioni 406.07, ikiwa ni moja ya miradi mikubwa ya maji kuwahi kutekelezwa nchini Tanzania.
![]() |
Mbali na kuleta faraja kwa wananchi, mradi huu unatarajiwa kuimarisha shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo hayo kwa kuwa upatikanaji wa maji ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya sekta hizo. Aidha, unatarajiwa kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Serikali imeahidi kuendelea kusimamia miradi mingine ya maji nchini ili kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji pia Rais Samia amewasisitiza wananchi wanaunganisha huduma ya maji pamoja na kulipa bili za maji kulingana na matumizi yao.
Uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni ishara nyingine ya jinsi serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza miradi mikubwa kwa lengo la kuboresha maisha ya Watanzania na kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika kwa wote.
Comments
Post a Comment