ANNE KILANGO AZINDUA KAMPENI SAME MASHARIKI KWA KISHINDO

ANNE KILANGO AZINDUA KAMPENI SAME MASHARIKI KWA KISHINDO.

Na Musa Mathias,
Same, Kilimanjaro.

Kwa shamrashamra na hamasa kubwa za kisiasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Same jana Septemba 2, 2025 kimezindua rasmi kampeni za uchaguzi katika eneo la Maore, Kata ya Maore, Jimbo la Same Mashariki, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro. Mamia ya wananchi walijitokeza kushuhudia tukio hilo lililoambatana na muziki, nderemo na hotuba za viongozi wa chama hicho.

Katika uzinduzi huo, mgombea ubunge wa CCM jimbo hilo, Mhe. Anne Kilango Malecela, alitambulishwa rasmi sambamba na madiwani 14 wanaowania nafasi katika kata mbalimbali.

Mgombea Ubunge Jimbo la Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela akihutubia wananchi walijitokeza kushuhudia uzinduzi wa kampeni jimboni humo. 

Akihutubia wananchi, Mhe. Anne Kilango aliahidi kuwa endapo atachaguliwa tena, kipaumbele chake kikubwa kitakuwa kuhakikisha barabara ya Mkomazi–Same yenye zaidi ya kilomita 100 inajengwa kwa kiwango cha lami.

Alibainisha kuwa tayari mkataba wa awamu ya kwanza kutoka Mkomazi hadi Ndungu umeshasainiwa, na ujenzi wa kilomita 36 unaendelea kwa ufadhili wa zaidi ya shilingi bilioni 59 zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Endapo nitarejea Bungeni, jambo la kwanza nitakaloanza nalo ni kushinikiza Mkandarasi aliyepo arudi kazini kukamilisha kipande cha kilomita 5, na kuendelea na awamu ya pili kutoka Maore hadi Same, yenye zaidi ya kilomita 56. Huu ni mradi mgumu unaohitaji mbunge mwenye sauti imara na uzoefu,” alisema Kilango huku akishangiliwa na umati.

Mbunge huyo pia aliitaja sekta ya kilimo kama mhimili wa maendeleo wa jimbo hilo, akisisitiza kuwa asilimia 72 ya tangawizi inayotumika nchini huzalishwa Same Mashariki, hivyo barabara hiyo itakuwa kiunganishi muhimu katika kukuza uchumi wa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Akigusia maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia, Kilango alisema:

“Wakati Rais Samia anaingia madarakani, jimbo letu lilikuwa na kituo cha afya kimoja pekee. Lakini ndani ya miaka minne ametujengea vituo vya afya vinne vipya, kuboresha kituo cha Ndungu na pia kufanikisha ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari. Haya ni mafanikio makubwa tunayopaswa kuyathamini.”

Viongozi wa CCM waliwahimiza wananchi wa Same kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku wakitoa wito wa kudumisha amani, mshikamano na mshikikiano bila kujali tofauti za kisiasa.

Kwa mujibu wa ratiba ya NEC, wananchi wa Same Mashariki pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, wanatarajiwa kupiga kura mwezi Oktoba mwaka huu ili kuwachagua rais, wabunge na madiwani watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.












Imeandikwa na Musa Mathias. 

Mwisho.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO