MAJIKO BANIFU KUPUNGUZA MATUMIZI YA MKAA NA KUNI MBEYA
📌 *Majiko banifu 9,330 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku mkoani Mbeya*
📌 *Wilaya Sita kunufaika na mradi*
📌 *Kila Wilaya kupata majiko 1,555*
📍 *MBEYA*
Serikali ya Mkoa wa Mbeya kupitia Katibu Tawala wa Mkoa Ndugu, Rodrick Mpogolo leo Jumanne Septemba 2, 2025 imepokea mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 9,330 yenye ufanisi mkubwa katika utumiaji wake.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya mradi Mhandisi wa miradi kutoka wakala wa nishaji vijijini (REA), Raya Majallah amesema,
Kupitia utafiti uliofanyika 2016 unakadiria kuwa takribani watu 33,024 hufariki kabla ya wakati kila mwaka hii ni sawa na asilimia 8.49 ya vifo vyote nchini Tanzania, kutokana na magonjwa ambayo yanachangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba wakati wa upikaji kwa kutumia nishati isiyo safi na salama.
Hivyo kwa kutambua hilo, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeaanda mpango wa uuzaji na usambazaji majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ili kupunguza athari za kiafya na mazingira zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo salama na pia kufikia lengo la serikali mpaka ifikapo 2034 zaidi ya asilimia themanini 80% ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Katika kufanikisha hilo, Wakala wa Nishati Vijijini unatarajia kusambaza na kuuza majiko 9,330 mkoa wa Mbeya katika wilaya sita za Busokelo, Chunya, Kyela, Mbarali, Rungwe na Mbeya Vijijini ambapo kila wilaya itapata majiko 1,555.
Mhandisi Raya ameendelea kwa kusema, mikataba ya mradi ilisainiwa tarehe 09 Mei, 2025 kati ya REA na mtoa huduma Kampuni ya Envotec Services Limited na itatekelezwa ndani ya miezi 15.
Mradi unatarajia kugharimu zaidi ya TZS Milioni 471.9 kwa mkoa wa Mbeya pekee, ambapo serikali itatoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na zaidi ya TZS Milioni 401.1 hivyo badala ya jiko kuuzwa kwa bei ya awali ya TZS 50,580 litauzwa kwa bei ya TZS 42, 993 na mwananchi atachangia 7,587 tu.
Kwa upande wake katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Ndugu Rodrick Mpogolo amesema, usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku ni sehemu ya Jitihada za serkali katika kuhamasisha na kuwawezesha wananchi kutumia nishati safi na salama za kupikia ili kuboresha Afya za wananchi na utunzaji wa mazingia hususan katika kukabiliana na ukataji wa miti ovyo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment