REA. YAENDELEA KUTEKELEZA KWA VITENDO MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
📌 *Majiko banifu 4,836 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku mkoa wa Njombe*
📌 *Jiko moja kuuzwa kwa bei ya ruzuku ya TZS 8,850 tu* .
📌 *Kila walaya kupata majiko 1,209*
📍 *NJOMBE*
Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari amekutana na Timu ya Wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) leo Septemba 1, 2025 na kupata taarifa ya mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku ambao unatarajia kuanzia mapema mwezi wa 9, 2025.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi wa miradi Kutoka wakala wa Nishati Vijijini, Raya Majallah, amesema,
Wakati Taifa likiwa kwenye mkakati wa kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia, Wakala wa Nishati Vijijini umekuja na mpango wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku yanayotumia kuni na mkaa mchache sana na yenye ufanisi mkubwa katika matumizi yake.
Mradi huu umekuja kwa lengo la kuimarisha na kuboresha Afya za wananchi, Mazingira, kukuza upatikanaji wa Nishati Safi na Endelevu, kupanua usambazaji wa nishati mbadala katika maeneo ya Vijijini na zaidi kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi kupitia teknolojia za kisasa na bora za kupikia.
Mhandisi Raya ameendelea kwa kusema, Serikali kupitia wakala wa Nishati Vijijini umeandaa mpango huu wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la zaidi ya asilimia themanini 80% ya watanzania ifikapo mwaka 2034 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mradi huu unatarajia kugharimu kiasi cha zaidi ya TZS Milioni 285.3 kwa mkoa wa Njombe pekee na utafanikisha uuzaji na usambazaji wa majiko banifu 4,836.
Uuzaji na usambazaji wa majiko banifu utafanyika katika wilaya nne (4) za mkoa wa Njombe ambazo ni wilaya ya Njombe, Ludewa, wanging’ombe na wilaya ya Makete ambapo kila wilaya majiko banifu 1,209 yatasambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku.
Mikataba ya mradi huu ilisainiwa tarehe 25 Julai, 2025 kati ya REA na mtoa huduma kampuni ya Envotec Services Limited.
Mtoa huduma atasambaza na kuuza majiko banifu kwa bei ya ruzuku katika wilaya zote nne. Gharama ya jiko moja ni TZS 59,000 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na TZS 50,150 hivyo mwananchi atanunua kwa gharama ya TZS 8,850 tu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari, ameishukuru na kuipongeza REA pamoja na mtoa huduma kwa kutumia fursa na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa majiko banifu ambayo yatauzwa kwa bei ya ruzuku kwa wananchi wa mkoa wa Njombe na hivyo kuchochea matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Comments
Post a Comment