MRADI WA MAJIKO BANIFU WATAMBULISHWA KIGOMA
📌 *Majiko banifu 8,424 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku mkoani Kigoma*
📌 *Wilaya Sita kunufaika na mradi*
📌 *Kila Wilaya kupata majiko 1,404*
📍 *KIGOMA*
Wakazi wa Kigoma waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia
Wito huo umetolewa leo Septemba 04, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Simon Nyakoro Sirro wakati akipokea mradi wa uuzaji na usambazaji wa majiko banifu unaosimamiwa na kuratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) .
"Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama katika kutunza mazingira na kuboresha Afya za wananchi" amesema Mkuu wa mkoa Mhe. Sirro, alipokuwa akipokea mradi huo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa mkuu wa mkoa, Mhandisi wa Miradi kutoka wakala wa Nishati Vijijini (REA), Raya Majallah amesema,
“Mradi huu unalenga kusambaza majiko banifu ili kukuza upatikanaji wa Nishati safi na endelevu, kupanua usambazaji wa Nishati mbadala katika maeneo ya vijijini na hivyo kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi kupitia teknolojia za kisasa na bora za kupikia.
Katika kufanikisha hilo, Wakala wa Nishati Vijijini umekuja na mpango wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku.
Mradi huu unagharimu kiasi cha zaidi ya TZS 429.5 ambapo serikali itatoa ruzuku ya TZS 365.1 na kufanikisha usambazaji na uuzaji wa majiko 8,424.
Uuzaji na usambazaji wa majiko banifu utafanyika katika wilaya Sita (6) za mkoa wa Kigoma ambazo ni wilaya ya Buhingwe, Kakonko, Kasulu, Kibondo, Kigoma Vijijini na wilaya ya Uvinza na kila wilaya kupata majiko 1,404.
Mikataba ya mradi huu ilisainiwa tarehe 09 Mei, 2025 kati ya REA na mtoa huduma kampuni ya Envotec Services Limited. Mtoa huduma atazambaza na kuuza majiko banifu kwa bei ya ruzuku katika wilaya zote Sita.
Gharama ya jiko moja ni TZS 50,990 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na TZS 43,341.50 na hivyo mwananchi atanunua jiko kwa kiasi cha TZS 7,649 tu.
Kwa upande wake Afisa masoko wa Kampuni ya Envotec Services Limited, Bi Kisa Sefa Mwamwaja amesema, majiko haya banifu yametengenezwa kwa kutumia Teknolojia za kisasa ambazo hazihitaji matumizi makubwa ya kuni na mkaa wakati wa kupika na hivyo kusaidia katika utunzaji wa mazingira.
Comments
Post a Comment