DC KASILDA APONGEZA UJENZI WA SOVAVI SEKONDARI: “NI UWEKEZAJI KWA TAIFA”
Na Ashrack Miraji
Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Sovavi iliyopo Kata ya Hedaru, wilayani Same, umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2025. Mradi huo unatajwa kuwa suluhisho muhimu kwa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa eneo hilo, ikiwemo kutembea umbali mrefu kwenda shule na msongamano mkubwa katika Shule ya Sekondari Mkombozi.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, aliyeongozana na Kamati ya Usalama ya Wilaya kukagua maendeleo ya ujenzi huo. Mhe. Kasilda amepongeza hatua iliyofikiwa na kutoa wito kwa mafundi pamoja na Kamati ya Ujenzi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Ujenzi wa shule hii ni kielelezo cha jitihada za serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu, jambo linaloendana na azma ya kitaifa ya kuinua viwango vya ufaulu na kukuza rasilimali watu wa taifa. Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ili wanafunzi waweze kunufaika kwa ubora,” alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka zote za ujenzi, kuzingatia viwango vilivyowekwa na kuhakikisha kila hatua inatekelezwa kwa umakini mkubwa. Amesema ameridhishwa na kazi iliyofanyika hadi sasa, huku akieleza matumaini kuwa mradi utakamilika kwa ubora unaotarajiwa.
Kwa upande wake, Mwl. Bakari Nyambwiro, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkombozi, amesema kukamilika kwa Sovavi Sekondari kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule yao pamoja na kupunguza umbali wa kutembea kwa wanafunzi kutoka maeneo ya jirani.
“Shule hii mpya itaimarisha mazingira ya kujifunza na kufundisha, hivyo kusaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wetu,” alieleza Mwl. Nyambwiro.
Kwa mujibu wa takwimu za mradi, serikali kupitia mpango wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu imetoa zaidi ya shilingi milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo. Hadi sasa, zaidi ya milioni 565 zimeshatumika, na kiasi kilichobaki cha takribani milioni 19 kimetengwa kwa ajili ya kumalizia kazi zilizosalia.
Mhe. Kasilda Mgeni pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kila mtoto nchini kupitia uboreshaji wa miundombinu na huduma za msingi mashuleni.
Comments
Post a Comment