UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI SOVAVI WAFIKIA ASILIMIA 85, UNATARAJIWA KUKAMILIKA SEPTEMBA 30
UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI SOVAVI WAFIKIA ASILIMIA 85.
Na Christina Thomas.
Same, Kilimanjaro.
Ujenzi wa mradi wa shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Hedaru (Sovavi Sekondari) iliyopo wilayani Same umefikia asilimia 85 ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2025, jambo linalotajwa kuwa suluhisho kubwa kwa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa eneo hilo ikiwemo kutembea umbali mrefu kwenda shule na msongamano katika Shule ya Sekondari Mkombozi.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, Septemba 3, 2025, alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo akiambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Same, Bi. Kasilda Mgeni akikagua moja ya dirisha katika majengo ya shule mpya ya sekondari ya kata ya Hedaru (Sovavi sekondari). Picha na Musa Mathias. |
Mhe. Mgeni amewataka mafundi na Kamati ya Ujenzi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa, akisisitiza kuwa serikali itaendelea na dhamira yake ya dhati ya kuboresha miundombinu ya elimu, kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanafunzi, na kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi sawa ya kujifunza katika mazingira bora.
"Ujenzi wa shule hii ni kielelezo cha jitihada za serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu, jambo linaloendana na azma ya kitaifa ya kuinua viwango vya ufaulu na kukuza rasilimali watu wa taifa, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya Elimu ili wanafunzi waweze kunufaika kwa ubora" alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka zote za ujenzi, kuzingatia viwango vilivyowekwa, pamoja na kuhakikisha kila hatua inafanyika kwa umakini. Amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa hadi sasa na ana imani mradi utakamilika kwa ubora unaotarajiwa.
Kwa upande wake, Mwl. Bakari Nyambwiro, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkombozi, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, jambo litakalosaidia kuinua viwango vya ufaulu wa wanafunzi.
Amesema pia shule hiyo mpya itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mkombozi pamoja na kupunguza umbali wa kutembea kwa wanafunzi wa maeneo ya jirani.
Kwa mujibu wa takwimu, serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 584 za Kitanzania kwa ajili ya mradi huo, ambapo hadi sasa zimetumika zaidi ya milioni 565 na kubaki shilingi zaidi ya milioni 19 kwa ajili ya kumalizia kazi zilizobakia.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mkakati wake wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini.
Comments
Post a Comment