KAMISHNA BADRU AFUNGUA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA MAKAZI ONLINE PORTAL*
📍Arusha | Tarehe 4 Oktoba, 2025.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro Bw Abdul-Razak Badru amefungua mafunzo kwa wadau wa uwekezaji katika sekta ya utalii kuhusu mfumo mpya wa kidijitali wa Makazi Online Portal (MoPO) kwa lengo la kuongeza uwazi na usawa katika upangaji wa makambi ya kulala wageni (Campsites) hususan eneo la Ndutu Ngorongoro
Akifungua mafunzo hayo Kamishna Badru ameeleza kuwa hatua ya kubuni mfumo mpya wa Makazi Online Portal inalenga kuboresha huduma kwa wateja katika sekta ya uhifadhi na utalii kwa kujikita kwenye matumizi ya teknolojia kwa huduma ambazo wadau hao wanazihitaji katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
“Mfumo tulioubuni kwa dunia ya sasa ni muhimu katika kuboresha huduma kwa misingi ya uwazi, haki na ufanisi, tunaamini kila mdau atapata huduma nzuri na kwa wakati bila upendeleo,” alisema Kamishna Badru.
Wakati wa mafunzo hayo Wataalam wa TEHAMA na Uwekezaji walitoa semina kwa washiriki kuhusu matumizi ya mfumo wa Makazi Online Portal ikihusisha namna ya kuomba nafasi za makambi, kufuatilia maombi, na kupata taarifa ya maombi yao kwa wakati.
Mfumo wa Makazi Online Portal uliohudhuriwa na wadau wa uwekezaji katika sekta ya utalii zaidi ya 150 unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu katika kuomba kuwekeza makambi ya kulala wageni eneo la Ndutu tofauti na mfumo wa zamani wa kutuma barua ya maombi kwa kamishna wa Uhifadhi hali inayoongeza uwazi wa kufuatilia maombi na ufanisi katika upangaji wa kambi hizo.
Comments
Post a Comment