MANISPAA YA KIBAHA IMETOA TSH MILIONI 420 KUTATUA CHANGAMOTO YA BARABARA ZA MITAA



KIBAHA: Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa jumla ya Shilingi Milioni 420 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kutengeneza na kufungua barabara za mitaa katika kata zote za manispaa hiyo, ikiwa ni hatua ya kutatua changamoto ya ya miundombinu ya barabara.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema Tayari kata zote Manispaa ya Kibaha zimepokea mgao wa Shilingi Milioni 30 Kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uboreshaji wa barabara ili kurahisisha huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Kupitia mapato yetu ya ndani, tumeamua kuwekeza katika barabara za mitaa kwa kuwa ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya wananchi. Kila kata sasa ina Shilingi Milioni 30 kwa ajili ya miradi hii na tutaendelea kusimamia utekelezaji wake kwa karibu,” amesema Dkt. Shemwelekwa.


Katika Kata ya Sofu, wananchi wameipokea kwa furaha hatua hiyo na wamepongeza uongozi wa Manispaa kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kutatua kero ya barabara.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Twendepamoja Mhe Idd Alfan amesema, “Wananchi wamehamasika sana kuona kodi wanazotoa zinatumika moja kwa moja kuboresha maisha yao. Mradi huu umewapa motisha zaidi ya kulipa kodi kwa hiari kwa sababu wanaona matokeo yake.”

Mwananchi wa Kata hiyo, Bi. Deborah Mkoma, amesema barabara zinazotengenezwa ni muhimu sana kwa kuwa zinapitika kuelekea hospitalini na maeneo mengine ya huduma muhimu.

“Kuna sehemu magari yalikuwa hayawezi kufika kabisa kutokana na ubovu wa barabara, lakini sasa hata bodaboda wanafika bila shida na kwa bei nafuu. Tunampongeza sana Mkurugenzi kwa juhudi zake,” alisema Bi. Mkoma.

Wananchi wa Manispaa ya Kibaha kwa ujumla wameonyesha matumaini makubwa kuwa mradi huu utaleta mabadiliko makubwa katika maisha yao ya kila siku na wameahidi kuendelea kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO