MGOMBEA URAIS CCM AFANYA MIKUTANO 21, AZIDI KUNADI SERA KWA HESHIMA NA UTULIVU


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa mgombea wake wa nafasi ya Urais tayari amefanikisha mikutano zaidi ya 21 ya kampeni katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, akiwa katika harakati za kunadi sera za chama hicho kwa njia ya kistaarabu, yenye kuzingatia maadili, utu na mshikamano wa kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa leo, Oktoba 5, 2025, jijini Dodoma na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa kampeni zinazoendelea kufanywa na mgombea huyo kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Kihongosi amesema kuwa ziara hizo zimekuwa chachu ya matumaini kwa Watanzania, kwa kuwa zimejikita katika kuelezea vipaumbele vya maendeleo ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuboresha uchumi, elimu, afya, miundombinu na ajira kwa vijana.

“Mgombea wetu anaendelea kusikiliza kero za wananchi kwa karibu, na kutoa majibu ya sera zinazotekelezeka. Amekuwa mstari wa mbele kuonyesha aina ya uongozi wa kivitendo, usiokuwa wa porojo bali wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kila Mtanzania,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa hadi sasa mgombea huyo ameshatembelea mikoa kadhaa ikiwemo Mbeya, Iringa, Mtwara, Lindi, Pwani, Arusha, Tanga, Dodoma, Unguja na Pemba, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kumkaribisha na kusikiliza maelezo ya sera za CCM kwa mwaka 2025 na kuendelea.

Kwa mujibu wa Kihongosi, kampeni hizo zimekuwa za kistaarabu na hazijajikita katika siasa za matusi au kejeli, bali zimebeba ujumbe wa matumaini, mshikamano, na maendeleo jumuishi ya taifa.

Aidha, ameeleza kuwa kuanzia Oktoba 7, 2025, mgombea huyo ataendelea na ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Simiyu, Mwanza na Mara, ambapo atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, kuwasilisha sera na kuelezea kwa kina dhamira ya CCM ya kuijenga Tanzania ya kisasa na yenye ustawi wa kiuchumi.

“Tunawaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo, wakimsikiliza mgombea wetu ambaye amejidhihirisha kuwa ni kiongozi mwenye dira, busara na uwezo wa kuyaongoza mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wote,” alisisitiza.

Amehitimisha kwa kusema kuwa CCM itaendelea kuendesha kampeni zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, huku ikihimiza amani na mshikamano kwa kila hatua ya mchakato wa uchaguzi

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO