NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi
NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi
Na Musa Mathias,
Same - Kilimanjaro.
Katika msimu huu wa mitihani, upepo wa matumaini na hamasa mpya umevuma katika shule za sekondari wilayani Same mkoani Kilimanjaro, baada ya Benki ya NMB Tawi la Same kushirikiana na wadau wa elimu kuwatia moyo wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha pili wanaotarajia kuanza mitihani yao ya kuhitimu hivi karibuni,
Kupitia tukio lililojawa na furaha na matumaini, Meneja wa NMB Tawi la Same, Bw. Saad Masawila, aliwasihi wanafunzi hao kusimama imara katika safari yao ya kielimu kwa kujikita kwenye misingi ya bidii, nidhamu na malengo thabiti.
“Soko la ushindani wa kielimu limekuwa kubwa sana,” alisema Bw. Masawila kwa msisitizo. “Tunataka kuona wanafunzi wetu wengi wakifanya vizuri wapate division one, na hata kama itatokea changamoto, basi wasishuke chini ya division three. Mafanikio ni matokeo ya juhudi, si bahati.”
Katika kuonyesha mshikamano na ari ya kuinua elimu, benki hiyo iliwakabidhi wanafunzi vitendea kazi mbalimbali vya masomo kama zawadi na motisha ya kuwaongezea hamasa wakati huu wa maandalizi ya mitihani. Tukio hilo lilipambwa na shangwe, tabasamu na maneno ya shukrani kutoka kwa wanafunzi walioguswa na moyo wa benki hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Same, Bi. Neema Lemunge, aliwataka wanafunzi hao kutumia muda uliosalia kwa makini, wakizingatia mafunzo waliyopatiwa darasani. Alisisitiza kuwa mafanikio hayaji kwa kubahatisha, bali ni matokeo ya nidhamu, kujituma na kujiamini.
“Mnaweza kufaulu kama mtaweka bidii na nidhamu,” alisema Bi. Lemunge. “Kila mmoja wenu ana nafasi ya kung’aa. Msiogope mitihani muione kama fursa ya kuonyesha matunda ya kazi yenu.”
Viongozi wa dini waliohudhuria waliongeza sauti zao, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha maadili mema, kumuomba Mungu, na kuzingatia heshima kwa wazazi na walimu. Walikumbusha kuwa mafanikio ya kweli hujengwa katika misingi ya imani, heshima na utu.
Katika hotuba ya shukrani, mmoja wa wanafunzi alizungumza kwa niaba ya wenzake, akieleza jinsi NMB imekuwa kama mzazi kwao.
“NMB si benki tu, bali ni rafiki na mlezi wetu,” alisema kwa shauku. “Kupitia misaada yao madawati, vifaa vya kujifunzia, elimu ya fedha, na sasa vitendea kazi wametufanya tuamini kuwa tunaweza kufika mbali.”
Mchango wa NMB katika elimu hauishii hapo. Benki hiyo imeendelea kutembelea shule mbalimbali za sekondari wilayani Same, ikiendesha programu za elimu ya fedha kwa vijana, huku ikisisitiza umuhimu wa nidhamu ya kifedha, bidii katika masomo, na mtazamo chanya kuhusu mafanikio ya baadaye.
Kupitia juhudi hizi, NMB imekuwa mfano bora wa taasisi ya kifedha inayogusa maisha ya wananchi kwa vitendo ikiweka msisitizo kwamba uwekezaji mkubwa zaidi si tu katika miundombinu, bali katika mtaji wa elimu na maarifa ya vijana.
Na kama alivyoeleza mmoja wa walimu wa shule hiyo kwa maneno ya busara “Kuna zawadi nyingi duniani, lakini hakuna yenye thamani kama elimu. Tunawashukuru NMB kwa kuona hilo na kulisimamia kwa moyo wa kizalendo.”



Comments
Post a Comment