DKT. MWIGULU; SERIKALI INATAMBUA NA KUTHAMINI MCHANGO WA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA UTALII NA UHIFADHI NCHINI
Mikumi - MOROGORO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi katika kuendeleza utalii na uhifadhi nchini.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Loji ya Mikumi Wildlife iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Mkoani Morogoro.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa loji hiyo utaongeza mvuto wa Hifadhi ya Mikumi na kuchochea ongezeko la watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi hiyo pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo katika Ukanda wa Kusini.
"Ujenzi wa hoteli hii ni wa viwango vya juu sana hongereni sana" Amesema Mhe. Dkt. Mwigulu
Aidha, ameahidi Serikali kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo viwanja vya ndege na barabara ili kuimarisha sekta hiyo. Amesema Serikali imeweka zaidi ya shilingi bilioni 35 kwa ajili ya kuboresha Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza utalii hasa wakati wa mashindano ya Mpira wa Miguu Barani Afrika (AFCON 2027).
Pia Mhe. Mwigulu ametoa rai kwa taasisi zote za Serikali kutumia muda mwingi kuwezesha wawekezaji Binafsi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji (Mb.) amesema ufunguzi wa loji hiyo utachangia kuongeza idadi ya watalii nchini, itakayochagiza kufikia malengo ya kufikisha watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, amesema hadi sasa idadi ya watalii imeendelea kuongezeka, ambapo imefikia watalii milioni 5.9 ikilinganishwa na watalii milioni 5.3 mwaka uliopita.
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa, Wizara inaendelea kuchukua hatua za kimkakati ikiwemo kuwahamasisha Watanzania na wageni kutoka nje ya Nchi kutumia fursa ya treni ya mwendokasi (SGR), kufungua lango jipya la kuingia Hifadhi ya Taifa Mikumi kupitia eneo la Chamgore, Kilosa.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa hoteli hiyo, mmiliki wa hoteli, Gullam ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano na namna inavyoendelea kuinua sekta binafsi, huku akiahidi kuendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii hapa nchini.






Comments
Post a Comment