WANAMICHEZO WA MALIASILI SPORTS CLUB WATAKIWA KUJITUMA NA KUDUMISHA NIDHAMU KWENYE MASHINDANO YA SHIMIWI -MWANZA



Na John Bera, Mwanza

Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii umewataka wanamichezo wanaoiwakilisha Wizara hiyo katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2025 kuzingatia nidhamu ya hali ya juu wanapotekeleza majukumu yao ya kimichezo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Utawala katika Wizara hiyo ambaye pia ni Mratibu wa Michezo Wizarani, Bi. Violeth Mlinga, wakati akizungumza na wachezaji wa  Maliasili Sports Club mara baada ya mazoezi ya asubuhi.

Bi. Mlinga amesema kuwa nidhamu ni nguzo muhimu katika Utumishi wa Umma na ndio msingi wa mafanikio ya kila mtumishi.

"Zingatieni sana nidhamu katika kila kitu, ikiwa ni wakati wa mazoezi, mashindano, pamoja na nje ya uwanja. Nidhamu ni chanzo kikuu cha mafanikio kwa mtumishi wa Umma," alisema Bi. Mlinga.

Aidha, amewahimiza wachezaji hao kujituma na kucheza kwa bidii, akisema juhudi zao zitaisaidia Wizara kuibuka na ushindi na hatimaye kusaidia juhudi za kuutangaza Utalii wa ndani na nje ya nchi.

"Tukumbuke kuwa tumekuja kupambana. Lengo ni kuiletea Wizara ushindi. Hivyo hakikisheni mnapambana kwa nguvu zote ili kuipa Wizara mafanikio, ambayo yatachochea pia utangazaji wa utalii wetu," aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu wa Maliasili Sports Club, Bw. Patrick Kutondolana, akizungumza kwa niaba ya wachezaji, alisema mashindano ya mwaka huu yana ushindani mkubwa, lakini timu zinaendelea kujiandaa kwa bidii kuhakikisha zinaleta ushindi.

"Mashindano ni magumu, lakini tumejipanga vizuri. Tutaendelea kujituma kwa bidii ili kuiwakilisha vyema Wizara na kuhakikisha tunachangia katika kutangaza utalii wa Tanzania." alisema Bw. Kutondolana.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO