WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA UVUNJIFU WA MAADILI NA KULIOMBEA TAIFA AMANI


Na,Agnes Mambo,Tanga .

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amewaomba viongozi wa dini kuendelea kukemea vitendo vya uvunjifu wa maadili pamoja na kuliombea taifa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Rai hiyo ameitoa wakati wa Baraza la Maulid Kitaifa la kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), lililofanyika wilayani Korogwe, mkoani Tanga. Waziri Mkuu amesema kauli za viongozi wa dini zina nguvu kubwa katika jamii, hivyo ni muhimu wakatumia nafasi hiyo kuhimiza maadili mema.

“Nawaomba viongozi wa dini muendelee kukemea na kutovifumbia macho vitendo vya uvunjifu wa maadili vinavyojitokeza katika jamii, hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Mhe. Majaliwa.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini pamoja na viongozi wao kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, kwa kuwa ushirikiano huo unasaidia kujadili changamoto kwa pamoja na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakary Zubeir, amewataka viongozi wa dini kote nchini kuhakikisha wanasimamia amani, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutokufumbia macho dalili au vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika maeneo yao, akisema kufanya hivyo ni kutekeleza malengo ya dini na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Mufti pia amewahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kujitokeza kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika upigaji kura ili kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameishukuru Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuchagua mkoa wa Tanga kuwa mwenyeji wa Baraza la Maulid Kitaifa.

Amesema Tanga ni mkoa wenye amani na utulivu, na utaendelea kuwa kielelezo cha mshikamano na usalama kwa wananchi wake.




Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO