SAFARI ZA TRENI MIKOA YA KILIMANJARO NA ARUSHA KUREJEA RASMI JUNI 18.
SAFARI ZA TRENI MIKOA YA KILIMANJARO NA ARUSHA KUREJEA RASMI JUNI 18.
Na Musa Mathias,
Kilimanjaro.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, ameendelea kusisitiza umuhimu wa Serikali kuharakisha mipango ya kuunganisha Mikoa ya Kaskazini na mtandao wa Reli ya Kisasa (SGR) ili wananchi wa maeneo hayo wanufaike na huduma bora za usafiri na uchukuzi kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini.
Akizungumza katika mahojiano wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Mhe. Makoi alisema ana matumaini makubwa kuona Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha ikiweka wazi mkakati wa kufufua reli ya Kaskazini au kujenga reli mpya ya kisasa ya SGR itakayounganisha Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine ya Kaskazini.
Makoi alieleza kuwa kwa sasa mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Kigoma, Tabora pamoja na baadhi ya mikoa ya Kusini imeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya reli, jambo ambalo limeongeza fursa za kiuchumi, biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo.
"Ni wakati sasa kwa Serikali kueleza wazi ni lini reli ya Kaskazini itafufuliwa rasmi au ni lini ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kuelekea mikoa ya Kaskazini utaanza, ili wananchi wa maeneo haya nao wanufaike na maendeleo haya makubwa yanayoendelea nchini," alisema Makoi.
Baada ya maombi hayo, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetangaza rasmi kurejesha huduma za usafiri wa abiria kwa kutumia treni za reli ya MGR kuelekea Mikoa ya Moshi na Arusha pamoja na Mwanza na Kigoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC, huduma hizo zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 18 Juni, 2026, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha na wananchi wa mikoa ya Kaskazini waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu kurejea kwa usafiri huo muhimu.
Wadau wa maendeleo katika ukanda wa Kaskazini wameeleza kuwa kurejea kwa huduma za treni ni hatua muhimu katika kuboresha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi, huku wakisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea na mipango ya muda mrefu ya kuunganisha ukanda huo na reli ya kisasa ya SGR.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ishara chanya kwa matarajio ya wananchi wa Kaskazini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitamani kuona eneo lao likiunganishwa na mtandao wa reli ya kisasa unaoendelea kujengwa nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafiri, biashara na uwekezaji
Mwisho.

Comments
Post a Comment