UJENZI WA BARABARA YA ITETE NJIWA–IPERA ASILIA WAPUNGUZA GHARAMA ZA USAFIRISHAJI WA MAZAO MALINYI
#Wananchi wanufaika baada ya gharama za kusafirisha gunia la mpunga kushuka kutoka Shilingi 15,000 hadi 3,000
Malinyi, Morogoro
Wananchi wa kata ya Njiwa wilayani Malinyi mkoani Morogoro wameanza kunufaika na matunda ya ujenzi wa barabara ya Itete Njiwa–Ipera Asilia uliotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kumeelezwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wananchi wa maeneo hayo baada ya kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafirishaji wa mazao hususan mpunga.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kijiji cha Njiwa, Bw. Plasdius Lihawa ambapo amesema umbali kutoka maeneo ya mashambani hadi makao makuu ya kata ni takribani kilomita 12 lakini hapo awali wananchi walilazimika kutumia hadi shilingi 30,000 kusafirisha mazao yao kutokana na ubovu wa barabara.
"Ilipokuja taarifa ya mradi huu wananchi walifurahi sana kwa sababu barabara ilikuwa changamoto kubwa kwetu. Kwa sasa baada ya ujenzi gharama zimepungua kwa kiwango kikubwa", amesema Bw. Lihawa.
Kwa mujibu wake, mabadiliko makubwa yameonekana zaidi katika usafirishaji wa mpunga ambapo zamani gunia moja lilikuwa likigharimu hadi shilingi 15,000 kulifikisha sokoni lakini sasa gharama hiyo imeshuka hadi kati ya shilingi 3,000 na 5,000.
Mbali na kupunguza gharama za usafirishaji ujenzi wa barabara hiyo pia umeongeza thamani ya mazao ya wakulima kutokana na urahisi wa kuyafikisha sokoni.
"Zamani mnunuzi alikuwa anaangalia kwanza gharama ya usafiri kabla ya kupanga bei ya mazao. Lakini sasa anaweza kufika kwa urahisi kununua mazao na kuyasafirisha kwenda sokoni bila shida na hii imeongeza thamani ya mazao yetu", amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Malinyi Mhandisi Charles Mang’ela amesema, kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kunyanyua tuta la barabara kilomita 3, uchongaji wa barabara kilomita 3 pamoja na ujenzi wa maboksi kalavati mawili.
Mhandisi Mang’ela amesema maboresho hayo yameongeza upatikanaji wa huduma za usafiri na mawasiliano kwa wananchi wa Itete Njiwa pamoja na Ipera Asilia.


Comments
Post a Comment