JOHN MALECELA: AMANI NI MSINGI WA KUKUZA UTALII NCHINI.

JOHN MALECELA: AMANI NI MSINGI WA KUKUZA UTALII NCHINI.

Na Musa Mathias. 
Same - Kilimanjaro. 

Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, John Samuel Malecela, amesema kuwa mafanikio ya sekta ya utalii duniani yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu, na kuwataka wananchi kuhakikisha wanailinda ili kuendeleza sekta hiyo muhimu kwa uchumi.
Malecela alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Same Utalii Festival lililofanyika katika viwanja vya stendi wilayani Same, mkoani Kilimanjaro. Alisisitiza kuwa utalii ni sekta muhimu inayochangia upatikanaji wa fedha za kigeni, huku baadhi ya nchi zikitegemea utalii kuendesha shughuli za serikali.

“Mahali penye amani ndipo watalii huvutiwa kuja. Hata kama kuna kitu kizuri kiasi gani, kukikosekana kwa utulivu huwafanya watu waogope kufika. Amani ndiyo msingi wa ukuaji wa utalii na uchumi wetu,” alisema Malecela.

Aidha, aliongeza kuwa ukarimu ni jambo la msingi katika kuvutia wageni, kwani baadhi ya maeneo hukosa watalii kutokana na kukosekana kwa moyo wa kuwakaribisha wageni.

Aliwahimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kuwa hayo ndiyo yatakayowezesha sekta ya utalii kukua na kuwanufaisha wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

HIFADHI YA NGORONGORO YASHIRIKISHA WATALII UZINDUZI WA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA.

NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi

ANNE KILANGO AZINDUA KAMPENI SAME MASHARIKI KWA KISHINDO