SEKTA YA MADINI YAENDELEA KUONGOZA THAMANI YA MTAJI WA UWEKEZAJI KUTOKA NJE.
Na Deborah Lemmubi-Kipeo Media Dodoma.
Wizara ya Madini imesema kuwa Sekta hiyo imeendelea kuongoza katika thamani ya mtaji wa Uwekezaji kutoka nje yani Foreign Direct Investment(FDI) katika mwaka 2024 ikiwa ni takribani ya robo tatu ya jumla ya mtaji wa Uwekezaji katika Sekta muhimu ikitokana na ripoti ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2025.
Ambapo pia ripoti hiyo inaonesha kiwango hicho cha mtaji kutoka nje katika Sekta hiyo kiliongezeka hadi kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024,kutoka dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na dola bilioni 8.64 mwaka 2022 ambapo ongezeko limechangiwa na uhamasishaji na uwepo wa mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Hayo yamesemwa mapema leo hii Aprili 27,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Madini Mhe Anthony Peter Mavunde wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha wa 2026/2027.
"Mhe Spika, Kulingana na ripoti ya uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025(Tanzania Investement Report 2025) Sekta ya Madini imeendelea kuongoza katika thamani ya mtaji wa uwekezaji kutoka nje (Foreign Direct Investment,FDI Stock) katika mwaka 2024 ikiwa ni takribani robo tatu jumla ya mtaji wa uwekezaji katika sekta muhimu".
"Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa kiwango cha mtaji kutoka nje katika Sekta ya Madini kiliongezeka hadi kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024 kutoka dola bilioni 9.15 mwaka 2023 ma dola bilioni 8.64 mwaka 2022".
Pamoja na hayo pia Wizara imeweka bayana mkakati wa vipaumbele vyake nane kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hatua ambayo inayolenga kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha rasilimali zinasimamiwa kwa ufanisi zaidi.
Ambapo Waziri Mavunde amesema serikali imejipanga kuimarisha utafiti wa madini ili kubaini maeneo mengine mapya yenye utajiri wa madini na kuongeza upatikanaji wa takwimu zilizo sahihi zitakazopelekea kuvutia zaidi wawekezaji.
Aidha amesema katika kuhakikisha Watanzania wananufaika katika sekta hiyo wizara inapanga kuongeza ushiriki wao katika mnyororo wa thamani wa madini hususan ni katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na wa kati kupitia mafunzo na uwezeshaji wa kitaalamu.
Ambapo serikali itaendelea kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo rasmi ya uchimbaji, mitaji pamoja na teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza shughuli zisizo rasmi.
Akizungumzia suala la mapato, Waziri Mavunde amesema kuwa juhudi zitaongezwa kudhibiti utoroshaji wa madini na kuhakikisha kodi na tozo zote zinalipwa ipasavyo, hatua itakayopelekea ongezeko lamapato ya serikalini.
Pamoja na kuimarisha masoko ya madini ili kuweka mazingira ya biashara yenye uwazi na ushindani wa haki, huku jitihada zaidi zikifanywa kuvutia uwekezaji kwa kuboresha sera na kurahisisha taratibu za utoaji wa leseni.

Comments
Post a Comment