KAMATI YA SIASA CCM SAME YAMPONGEZA MBUNGE ANNE KILANGO, YAHIMIZA ULINZI WA VYANZO VYA MAJI NA MIUNDOMBINU YA MAJI.

KAMATI YA SIASA CCM SAME YAMPONGEZA MBUNGE ANNE KILANGO, YAHIMIZA ULINZI WA VYANZO VYA MAJI NA MIUNDOMBINU YA MAJI.

Same, Kilimanjaro.

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same imempongeza Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango, kwa mchango wake mkubwa wa kuwasemea wananchi bungeni na kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi wa jimbo hilo.

Pongezi hizo zimetolewa Aprili 22, 2026, wakati kamati hiyo ilipofanya ziara maalum ya kukagua, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maji inayosimamiwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Same Mashariki.

Katika ziara hiyo, kamati imeitaka jamii kutambua na kuthamini jukumu lao la msingi katika kulinda miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vya maji, ikisisitiza kuwa wananchi ndio walinzi wa kwanza wa rasilimali hiyo muhimu kwa maisha na maendeleo yao.
Imeelezwa kuwa ushiriki wa wananchi katika ulinzi wa miundombinu hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaimarika na kuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Bi. Neema Adam amesema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha huduma ya maji vijijini, bado kuna changamoto mbalimbali zinazoathiri upatikanaji wa huduma hiyo.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wizi wa miundombinu ya maji kama mabomba, uchepushaji wa maji kinyume cha taratibu zilizowekwa, pamoja na shughuli za kibinadamu hususan kilimo kinachofanyika karibu na vyanzo vya maji.

Bi. Adam amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya wote, huku akiwahimiza viongozi wa chama na serikali kuanzia ngazi ya kata hadi vitongoji kuwa macho na kuchukua hatua za haraka kwa kutoa taarifa za siri wanapobaini vitendo vya uharibifu au hujuma dhidi ya vyanzo vya maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuharibu vyanzo vya maji na miundombinu ya maji. Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha afya na ustawi wa jamii, hivyo havitavumiliwa kwa namna yoyote ile.
Aidha, ameonya dhidi ya kuendelea kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo na ufugaji karibu na vyanzo vya maji, akieleza kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa kwa wote watakaokiuka maelekezo hayo. Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi ya maji ili kuboresha huduma hiyo, hivyo ni wajibu wa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda uwekezaji huo.

Katika hitimisho lake, Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Same imerudia kumpongeza Mhe. Anne Kilango kwa juhudi zake za dhati za kuwatumikia wananchi wa Same Mashariki.

Kamati hiyo imewasisitiza wananchi kuendelea kumuunga mkono mbunge huyo pamoja na juhudi za serikali ili kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanaendelea kudumishwa na kuwanufaisha wananchi wote wa jimbo hilo.











Imeandaliwa na @musamathiasnjogolo 
Mwisho.


#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX karibu sana.

Comments

Popular posts from this blog

HIFADHI YA NGORONGORO YASHIRIKISHA WATALII UZINDUZI WA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA.

NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi

ANNE KILANGO AZINDUA KAMPENI SAME MASHARIKI KWA KISHINDO