BALOZI BATILDA: TUIMARISHE MIFUMO, UTAYARI WA KUDHIBITI MAJANGA.


Na,Agnes Mambo,Tanga.

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, ametoa rai kwa taasisi za umma na binafsi mkoani humo, kuendelea kuimarisha mifumo na utayari wa kudhibiti majanga, ili yasiwaathiri watu na mali zao.

Ameyasema hayo leo Julai 26, 2025, alipotembelea kiwanda cha kampuni ya Mamujee Products Limited ambacho jengo lake moja liliteketezwa kwa moto usiku wa kuamkia jana.

Mhe Balozi Dkt Batilda aliyefuatana na Katibu Tawala Mkoa, Rashid Mchatta na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama (KU) ya mkoa huo, amesema mifumo na utayari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji umesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti madhara zaidi ambayo yangesababishwa na moto huo.


Mhe Balozi Dkt Batilda, alipata maelezo ya namna moto huo ulivyowaka na kudhibitiwa kwenye jengo hilo, hivyo kutoenea na kuathiri maeneo mengine ya kiwanda hicho kinachotengeneza mafuta ya kujipaka.

Maelezo hayo yalitolewa na Zimamoto, kisha Mhe Balozi Dkt Batilda alizungumza na askari wa jeshi hilo wa mkoani Tanga na waliotoka Kinondoni jijini Dar es Salaam, Pwani na vijana wa kujitolea walioshiriki kuuzima moto huo.

Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, weledi na umahiri wa wazima moto walioshiriki, umefanikisha ukoaji wa mali za kampuni hiyo hususani majengo, bidhaa na miundombinu mingine.


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Wilaya ya Tanga, Mrakibu Mwandamizi Kattala Issaka, amesema moto ulianza kuwaka majira ya saa tatu za usiku wa juzi na kwamba pamoja na mafanikio ya kuudhibiti, ipo haja kwa wawekezaji kuihusisha Zimamoto katika ujenzi na usimikaji wa miundombinu ili kutoa ushauri wenye tija pindi yanapotokea majanga kama moto.

Amesema moto ulioteketeza jengo la kiwanda hicho ungeweza kuenea na kuathiri maeneo mengine ikiwemo mtungi mkubwa wa gesi inayotumika kupikia (LPG), ofisi za utawala na maghala ya kuhifadhia bidhaa zinazozalishwa kiwandani humo, miongoni mwa mengine kadhaa.

Naye Meneja wa Kiwanda hicho, Ravi Thumpuri, ameupongeza uongozi wa Mkoa chini ya Mhe Balozi Dkt Batilda, kuwaunganisha wadau waliosaidia kuongeza nguvu na hatimaye kuudhibiti moto huo.


 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO