KAMISHNA BADRU AWAONGOZA WATUMISHI WA NCAA KWENYE MAKABIDHIANO YA MWENGE WA UHURU WILAYA ZA NGORONGORO NA KARATU.
Mwandishi wa NCAA, Karatu.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdulrazaq Badru amewaongoza watumishi wa Mamlaka hiyo kwenye makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya wilaya ya Ngorongoro na Karatu za mkoa wa Arusha.
Mwenge wa Uhuru umewasili katika wilaya ya Karatu ukitokea wilaya ya Ngorongoro ambapo ulikimbizwa katika wilaya hiyo tarehe 8 Julai 2025 na leo tarehe 9 Julai, 2025 umekqbidhiwa wilaya karatu kupitia geti kuu la Loduare lililopo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo aliukabidhi mwenge huo kwa mkuu wa wilaya ya Karatu Dkt. Lameck Karanga ambapo baada ya makabidhiano hayo ulianza mbio zake katika wilaya hiyo kwa kukagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Tukio hilo lilipambwa na burudani mbalimbali za wasanii kutoka makabila maarufu ya wilaya za Ngorongoro na Karatu ambayo ni Wamasai, Wadatoga, Wahadzabe na Wairaq na ujumbe uliosisitizwa na viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wakimbiza mwenge ni kuwataka wananchi kushiriki zoezi la uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025.
Ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni; "Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu"
Comments
Post a Comment