TFS YAPONGEZWA KWA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU KWA WAKATI


Mufindi, 22 Julai 2025

Wadau wa biashara ya mazao ya misitu wameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Shamba la Miti Sao Hill, kwa juhudi zake za kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati, hatua iliyowezesha kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara hiyo.

Pongezi hizo zilitolewa wakati wa kikao kati ya viongozi wa Umoja wa Wadau wa Uvunaji wa Mazao ya Misitu (UWASA) na uongozi wa TFS – Shamba la Miti Sao Hill, kilichofanyika leo katika ukumbi wa makao makuu ya shamba hilo mkoani Iringa.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa UWASA, Bw. Chesco Ng’umbi, alisema licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa katika mnyororo wa uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu, TFS imeendelea kuonyesha ushirikiano na kujibu changamoto hizo kwa wakati.

“Sisi kama wadau wa uvunaji katika Shamba la Sao Hill tunaishukuru TFS kwa kuwa sikivu na kushughulikia changamoto zetu kwa wakati. Ushirikiano huu umechochea maendeleo na kutuwezesha kufanya shughuli zetu kwa ufanisi,” alisema Bw. Ng’umbi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa elimu ya mara kwa mara kwa wadau kuhusu taratibu za kisheria katika biashara ya mazao ya misitu ili kuhakikisha shughuli hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kuepuka migongano isiyo ya lazima.

“Tunaomba TFS iendelee kutupatia elimu kuhusu biashara ya mazao ya misitu, hasa kuhusu taratibu na sheria. Vikao vya aina hii viendelezwe kwa ajili ya kujengeana uelewa wa pamoja,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoram, aliwataka wadau wa misitu kuhakikisha wanalipa vibali kwa wakati na kufuata utaratibu wa uvunaji na usafirishaji wa mazao hayo ili kuepuka migongano na taasisi za udhibiti.

“Mwaka wa fedha 2025/2026 umeanza. Tunawasihi waliopata migao ya uvunaji kuhakikisha wanakamilisha taratibu za ulipaji na uvunaji kwa wakati. Hii itachangia kuongeza mapato ya serikali kupitia TFS,” alisema Yoram.

Aliongeza kuwa mifumo inayotumika katika TFS inaunganishwa na taasisi nyingine, hivyo ni muhimu kwa wadau kuhakikisha nyaraka zao zinakuwa sahihi na halali wakati wote wa utekelezaji wa shughuli zao shambani.

“Tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mifumo inatakiwa kusomana. Hivyo, taarifa zisizolingana kati ya taasisi huleta mkanganyiko. Tuongeze uaminifu na usahihi wa nyaraka,” alieleza Yoram.

Aidha, alisisitiza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika biashara ya mazao ya misitu ili kuongeza tija, kurahisisha taratibu, na kuhakikisha wadau wanapata faida stahiki kupitia mfumo rasmi wa kibiashara.






 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO