MWALIMU PAWA AONGOZA WANAFUNZI WA KAZITA ZIARA YA MAFUNZO KWA VITENDO MAPANGO YA AMBONI TANGA



Mustapha Seifdine, Tanga.

Wanafunzi wa Shule la Msingi Kazita iliyoko Wilayani Muheza mkoani Tanga wakiongozwa na Mwalimu Jao Kalesi, maarufu kama Mwl. Pawa, wamefanya ziara ya mafunzo ya vitendo katika Mapango ya Amboni Tanga ambayo ni moja ya kivutio cha utalii kinachoelezea historia ya urithi wa utamaduni na harakati za kupigania uhuru nchini. 

Ziara hiyo ya mafunzo imelenga kuwapa nafasi wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu historia, urithi wa utamaduni na mambo kale pamona na kujifunza shughuli za uhifadhi, utalii na utunzaji wa mazingira. 

Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Huduma za Utalii na Masoko NCAA, Mariam Kobelo aliwashukuru walimu na wanafunzi wa shule ya Kazita kwa juhudi za kuendeleza elimu ya uhifadhi kwa vizazi vya sasa na vijavyo huku  akiwataka wawe mabalozi wazuri wa Mapango ya Amboni.


Kamishna Kobelo  amempongeza Mwl. Kalesi kwa ubunifu  wa kutumia nyimbo na  muziki, hususan wimbo maarufu wa msanii Mbosso “Pawa”, kufundishia wanafunzi na kuwahamasisha kujifunza kwa ari na vitendo.

Akiwa katika Mapango hayo Mwl. Kalesi ameahidi kuendelea kushirikiana na walimu wengine kutangaza mapango hayo na kuyatumia kama darasa la kujifunza kwa vitendo.

Afisa Uhifadhi Daraja la Pili na Mkuu wa Mapango ya Amboni, Ramadhan Rashid, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 hifadhi ya Mapango ya Amboni imepokea wageni 19,743 na mapato ya zaidi ya Tsh 40 milioni hali inayoonesha kuwa mapango hayo yana  mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa kupitia shughuli za utalii.


Mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Kazita Juma Omari Mchevu kwa niaba ya wenzake aliishukuru NCAA kwa kuwapa nafasi ya kutembelea mapango hayo na kuwataka wazazi wawapeleke watoto wao ili wajifunze kwa vitendo.

Mapango ya Amboni Tanga ni moja ya maeneo  yanayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo mamlaka hiyo imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii kwa ajili 
ya kuendelea kuvutia wageni wengi zaidi.




Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO