DKT. MATARAGIO AONGOZA WADAU UTOAJI MAONI MPANGO WA MATUMIZI YA GESI ASILIA NCHINI (NGUMP)*
*📌Unalenga Kuchochea matumizi ya Gesi Asilia nchini*
📌 *Kuainisha matumizi ya Gesi Asilia kwa sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka 25 kuanzia sasa*
📌Kuangazia masoko ya Gesi Asilia ndani na nje ya nchi*
📌Wadau waomba uharakishaji mikopo kwa wawekezaji Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia*
*DSM*
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amefungua warsha ya wadau iliyolenga kuchambua na kutoa maoni kuhusu Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia nchini (NGUMP) kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia sasa.
Mpango huo utaonyesha kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia kinachohitajika katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya viwanda, uzalishaji wa umeme, sekta ya usafirishaji pamoja na matumizi ya nyumbani
Warsha hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam imeandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na kuhusisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
"Mradi huu wa NGUMP utatuwezesha kufahamu kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali hivyo itakuwa rahisi kufahamu na kutenga kiasi cha gesi asilia inayohitajika katika eneo husika," amsema Dkt. Mataragio
Ameongeza kuwa NGUMP itasaidia kuona namna bora ya kuendeleza miundombinu ya gesi ya asilia nchini pamoja na kutafuta masoko ya gesi asilia ndani na nje ya nchi pia kuangalia mchango wa gesi hiyo katika uchumi wa nchi.
Vilevile amesema NGUMP itarahisisha utekelezaji wa DIRA ya Maendeleo ya 2050 kwa kuwa Gesi asilia ipo katika Sekta ya Nishati ambayo ni kichocheo cha pili Kati ya vitano vya kufanikisha matokeo ya Dira.
Aidha amesema NGUMP itatekeleza mpango mkakati wa Matumizi Nishati Safi ya Kupikia na Sera ya Nishati ya mwaka 2015.
Mhandisi John Bura ni mmoja ya washiriki katika warsha hiyo ambaye amesema kuwa mpango huo utasaidia kuchochea matumizi ya gesi asilia, pamoja na kuongeza kiwango cha matumizi ya gesi nchini.
Bura ameiomba Serikali pamoja na Taasisi za Fedha kuharakisha utoaji wa mikopo kwa wawekezaji hasa wa ndani wanaotaka kuwekeza katika maeneo mbalimbali kwenye sekta hiyo ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi kwa lengo la kupata matokeo mazuri yenye tija zaidi.
Hatua ya utoaji utoaji maoni ya NGUMP imefikwa baada Wizara ya Nishati na JICA kukamilisha rasimu ya NGUMP kupitia Mradi wa kujenga uwezo katika matumizi ya Gesi Asilia na kuongeza uzalishaji.
Comments
Post a Comment