WIZARA YA NISHATI YAKAGUA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA TAASISI ZINAZOLISHA WATU ZAIDI YA 100 ILEMELA



📌 *Lengo ni kuhakikisha Taasisi za Umma na Binafsi zinatekeleza agizo la Serikali la kutumia Nishati Safi ya Kupikia*

📌 *Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia ahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri/Manispaa kuhakikisha agizo hilo la Serikali linatekelezwa*

📌 *Awaasa Walimu kufundisha Wanafunzi juu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia*

Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia,  Nolasco Mlay pamoja na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati   wameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa lengo la kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

Ziara hiyo imeanza kwa kukagua  shule tatu za Sekondari katika Manispaa ya Ilemela ambazo zimeanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia baada ya kunufaika na mradi wa CookFund kupitia mpango wa kimataifa wa Integrated Approach to Sustainable Clean Cooking Solution unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).

Ziara hiyo pia inalenga kufanya tathmini ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazopokea ufadhili kutoka mradi wa CookFund.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Nolasco Mlay amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), ambao unalenga kuhakikisha taasisi za umma ikiwemo shule, zinatumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi.

Katika kuhakikisha kuwa agizo hilo la Serikali linatekelezwa kwa mafanikio, Mlay amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa ambao bado taasisi katika maeneo yao hazijahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi  ya kupikia kuhakikisha kuwa wanatekeleza Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia

"Taasisi za Umma na Binafsi katika maeneo yenu kama vile Shule, Hospitali, Magereza pamoja Jeshi zinapaswa kutumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi ili kuepusha athari za kiafya na kimazingira kwa nchi." Amesema Mlay

Sambamba na hilo,  Mlay amewahimiza Walimu na Wakuu wa Shule kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wanafunzi juu ya faida ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili wawe mabalozi  wa kuelimisha wengine.


“Tunawaomba walimu kuelekeza wanafunzi kuhusu matumizi ya gesi asilia, majiko banifu na umeme kama njia mbadala za kuni na mkaa kwani watoto hawa wanapojifunza, watasaidia kubadilisha mitazamo ya jamii zao kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi na kutumia nishati safi ya kupikia". Amesisitiza  Mlay

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Ilemela, Afisa Elimu Maalum wa Manispaa hiyo amepongeza utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia  unaoendelea katika Manispaa ya Ilemela akiahidi kuwa Manispaa hiyo itaendelea kutekeleza agizo hilo ambapo kwa sasa tayari kuna shule kumi ambazo zipo kwenye mpango huo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Vilevile, Walimu Wakuu wa Shule zilizokaguliwa wameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yamesaidia shughuli za upishi kufanyika katika mazingira rafiki na salama,  kuokoa muda  na kuwa na gharama nafuu.

Katika hatua nyingine,  Wataalam kutoka Wizara ya Nishati walitembelea shule ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia na kuwaasa Viongozi wa shule hizo zinazotegemea kuni na mkaa kuanza kuboresha mifumo yao ya upishi na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Shule tatu zilizotembelewa katika Manispaa ya Ilemela ambazo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia ni pamoja na Shule ya ufundi ya Wavulana ya Bwiru Sekondari, Shule ya Wasichana ya Bwiru Sekondari pamoja na Shule ya Sekondari ya Buswelu.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO