MHANDISI MATIVILA AMTAKA MKANDARASI ANAYEJENGA DARAJA LA MOHORO KUKAMILISHA UJENZI KWA WAKATI
Rufiji, Pwani
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amemtaka Mkandarasi anayejenga daraja la Mohoro (MAC CONTRACTORS COMPANY LTD) lenye urefu wa mita 100 wilayani Rufiji mkoani Pwani kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Mativila amesema fedha za mradi huo zipo hivyo, amemsisitiza Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi huo kumsimamia Mkandarasi akamilishe kazi hiyo kwa wakati ili kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa kata ya Mohoro.
"Mliomba fedha kutokana na kazi hii kuongezeka, Serikali imeongeza fedha 50% ili kazi hii ikamilike, zipo kazi ndogondogo zinaweza kuendelea kufanyika, hivyo nasisitiza kazi hii ikamilike kwa wakati", amesema.
Aidha, amewataka Wakandarasi wazawa wajitahidi kukamilisha miradi kwa wakati ili Serikali iendelee kufanya kazi nyingi na Wakandarasi wa Kitanzania badala ya kuwatumia Wakandarasi wa nje.
Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema ujenzi wa daraja la Mohoro wenye thamani ya Shilingi Bilioni 17 unatakiwa kukamilika tarehe 24 Machi, 2026 na amemsisitiza Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa daraja hilo likamilike kwa wakati ili wananchi waendelee kupata huduma katika maeneo yao.
"Mradi huu ukikamilika unaenda kuwasaidia wananchi wa Rufiji, shughuli nyingi za ukanda huu ni kilimo cha mazao mchanganyiko pamoja na viwanda hivyo kukamilika kwa daraja hili kutaongeza uzalishaji", amesema.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Emmanuel Mahimbo amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 50 ambapo wameshakamilisha ujenzi wa boksi kalavati mbili, nguzo nne na kuinua tuta la barabara ambapo ameeleza uchelewaji wa kazi umetokana na athari ya mafuriko ya mwaka jana pamoja na kupitia tena usanifu wa daraja hilo.
Nao, wakazi wa Mohoro, wameeleza furaha yao, wakisema daraja hilo litawasaidia wakazi wa vijiji vya Mohoro na Chumbi kusafirisha bidhaa zao, litaepusha vifo vinavyosababishwa na mamba, litasaidia akina mama kujifungua hospitalini na kurahisisha usafiri wa watoto kwenda shule.
Comments
Post a Comment