DC KASILDA AWAKA UTIRIRISHAJI MAJITAKA YA KIWANDANI KUELEKEA MTONI
DC KASILDA AWAKA UTIRIRISHAJI MAJITAKA YA KIWANDANI KUELEKEA MTONI
Na Musa Mathias,
Same, Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amepiga marufuku mara moja utiririshaji wa maji machafu yenye kemikali kutoka Kiwanda cha kuchakata mkonge mali kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MELT) kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hassan Sisal Estate katika kata ya Makanya kwenda kwenye mto unaotumika na wananchi kwa shughuli za kilimo, mifugo na matumizi mengine ya kibinadamu.
Agizo hilo limetolewa kufuatia wasiwasi wa uchafuzi wa mazingira na athari kwa afya za wakazi wa Makanya na maeneo mengine yanayopata maji kupitia mto huo, ambapo awali Mhe. Kasilda alitembelea baadhi ya maeneo na kujionea hali ya maji kwenye mto yaliyokuwa na rangi nyeusi yanayotoa harufu kali, hali iliyomlazimu kufika kiwandani ili kujiridhisha na chanzo cha uchafuzi huo.
Pia, amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha kuwa wataalam wa mazingira na afya wanakwenda kufanya uchunguzi wa kina kuhusu hali ya mazingira katika kiwanda hicho, kutokana na viashiria vya ukiukwaji wa sheria za kimazingira ili sheria ziweze kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 129 kinakataza mtu yeyote kuachilia maji taka au taka hatarishi moja kwa moja kwenye mazingira bila kibali au matibabu sahihi.
Hata hivyo, viwanda vinapaswa kuwa na mitambo maalumu ya kutibu majitaka kabla ya kumwaga kwenye mazingira na endapo utatokea ukiukwaji mamlaka ya usimamizi wa mazingira (NEMC) Itachukua hatua.
Baadhi ya picha zikionesha maeneo mbalimbali ndani ya kiwanda cha kuchakata mkonge kilichopo kata ya Makanya wilayani Same. Picha na Musa Mathias.
Mwisho.
Comments
Post a Comment