RC BATILDA AKABIDHI MKATABA WA MRADI WA UMEME WA SH. BILIONI 20.5 KWA VITONGOJI 180 MKOANI TANGA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amekabidhi rasmi mkataba wa mradi wa usambazaji wa umeme katika vitongoji 180 vinavyopatikana katika majimbo 12 ya uchaguzi mkoani humo.
Amesema Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia kampuni ya Transpower kwa gharama ya shilingi bilioni 20.5.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mkataba kwa mkandarasi, Mhe. Dkt. Batilda alitoa wito kwa wakandarasi wanaopata zabuni za kazi katika mkoa huo kuhakikisha wanatenga nafasi za ajira kwa vijana wa maeneo husika, ili wanufaike moja kwa moja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunatamani sana vijana wapate ajira katika miradi hii, na nitoe msisitizo—nitapita kukagua kazi zinazofanywa, nikute vijana wa Tanga wapo,” alisisitiza Mhe. Dkt. Batilda.
Mkuu wa mkoa huyo, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo nishati ya umeme, ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.
Balozi Dkt. Batilda aliwataka REA kushirikiana na TANESCO kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati, ili wananchi wa vitongoji husika wapate huduma hiyo muhimu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwema, alisema serikali imeamua kuwekeza fedha nyingi kwenye sekta ya umeme kwa kuwa ni nishati ya msingi katika maisha ya kila siku na maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkandarasi kutoka kampuni ya Transpower, Cathbet Shirima, aliahidi kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya muda uliopangwa.
Comments
Post a Comment