Wananchi wa Lambo waishukuru serikali kwa kuwapatia ardhi ya Makazi

WANANCHI WA LAMBO WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWAPATIA ARDHI YA MAKAZI.

Na Mwandishi Wetu, 

Hai, Kilimanjaro. 

Kaya 78 za Kitongoji cha Lambo, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, ziliokuwa zikikabiliwa na changamoto ya ardhi zimeishukuru serikali kwa kuwapatia ekari 156 za ardhi kwa ajili ya makazi. 

Wananchi hao ambao zamani walikuwa ni wafanyakazi wa shirika la umma la mkonge, Lambo Estate mwaka 1970, walikuwa

wakikabiliwa na changamoto ya ardhi pamoja na makazi ya kudumu baada ya mwekezaji kushindwa kuwahudumia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, wamesema walikuwa wakiishi katika mazingira magumu baada ya mwekezaji kushindwa kuwahudumia na kwamba walikosa mahali pa kuishi na kuishi katika mazingira magumu.

Nyumba walizokuwa wakiishi awali baadhi ya wafanyakazi wa shirika la Mkonge, Lambo Estate, katika kitongoji cha Lambo, Wilaya ya Hai kabla ya kupewa ardhi ya makazi.



Aidha, wamesema hatua ya serikali kuwapatia ardhi ya makazi ya kudumu si tu imewapa utulivu wa maisha, bali imewajengea mazingira ya kufanya shughuli za maendeleo kwa uhuru na kujiinua kiuchumi.

Augustino Mwakatumbule, mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho, amesema wanaishukuru serkali kwa kuwapatia ardhi kwa ajili ya makazi na kwamba kwa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya makazi ya kuishi.

"Mwanzoni tulishindwa kufanya uendelezaji wowote wa makazi kutokana na kwamba tulikuwa hatuna mahali pakujenga, tulijenga vijumba vidogo vidogo ambavyo havina ubora, lakini sasahivi baada ya kupatiwa maeneo na serikali, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya makazi ya kuishi,"amesema Mwakatumbule.

Baadhi ya makazi ya wananchi wa kitongoji cha Lambo, Wilaya ya Hai baada ya kupewa ardhi ya makazi na serikali na kufanya uendelezwaji wa nyumba za kisasa.


Mkazi mwingine wa kitongoji hicho, Magreth Gunda amesema baada ya kupatiwa ardhi hiyo wameweza kufanya uendelezwaji mkubwa wa makazi na kwamba huduma zote za kijamii kwasasa zinapatikana katika maeneo yao.

"Hatua hii ya serikali kutupa maeneo, imebadilisha maisha yetu kwa kiasi kikubwa kwani kwa sasa tunaishi kwenye makazi bora na huduma muhimu kama umeme na maji zinaendelea kuletwa katika maeneo yetu,'amesema Magreth 

Akizungumza Katibu wa wafanyakazi wa Lambo Estate, Said Mwaliko amesema mgawanyo huo wa ardhi utapunguza manung'uniko kwa wananchi hao ambao zamani walikuwa ni wafanyakazi wa Lambo Estate.

Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lambo, Vitalis Shamuhilu ameishukuru serikali kwa kutoa ardhi kwa ajili ya wananchi hao ambapo amesema serikali imetoa ekari mbili kwa kila kaya zipatazo 78.

"Serikali ilitoa ekari mbili mbili kwa kaya 78 zilizokuwa na uhitaji wa makazi, ambapo kwasasa hawa wananchi wamefanya maendeleo makubwa kwenye maeneo haya ambayo wanaishi kwa sasa,"amesema Mwenyekiti huyo 

Amesema “Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza juhudi hizi, hadi sasa wananchi waliowengi tayari wamejenga makazi yao na wengine wameshahamia," amesema Shamuhilu.

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO