DCEA YATOA MAFUNZO WILAYANI SAME KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.

DCEA YATOA MAFUNZO WILAYANI SAME KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.

Same, Kilimanjaro

Katika harakati za kitaifa za kuikomboa jamii dhidi ya janga la dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini, imeendesha mafunzo maalum kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi vitongoji wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Mafunzo hayo, yameyofanyika leo Mei 29, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same ambayo yamelenga kuwawezesha viongozi hao kutambua, kuzuia na kushughulikia changamoto zinazotokana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya, huku yakisisitiza maadili, uwajibikaji na ushirikiano wa kijamii katika mapambano hayo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, amesema kuwa dawa za kulevya si tu kwamba zina madhara ya kiafya kwa binadamu, bali pia zinachangia kudhoofisha uchumi, kuvuruga familia, kusababisha kuporomoka kwa maadili, kupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza matukio ya uhalifu.

Alisema: “Hili ni janga linalohitaji nguvu ya pamoja kuanzia viongozi, wazazi, walimu na vijana wenyewe ambao ndiyo waathirika wakubwa wa dawa za kulevya. Hivyo nawahimiza, kupitia mafunzo haya, mkawe mabalozi na waelimishaji, kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kupambana dhidi ya dawa za kulevya katika maeneo yenu.”


Aidha, amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha wanakuwa wawajibikaji, waadilifu na kutoshiriki au kufumbia macho biashara haramu ya dawa za kulevya katika maeneo yao, akibainisha kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Afisa Elimu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kaskazini, Ndg. Shaban Miraji, amesema kuwa sababu kuu zinazochangia matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na malezi duni, ukosefu wa elimu sahihi kuhusu madhara ya dawa hizo, pamoja na hali ngumu ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 inaeleza kuwa hukumu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa kulima bangi au mirungi, kufanya biashara, kusafirisha au kukutwa na bangi au mirungi isiyozidi kilo 100 kifungo cha maisha zikizidi kilo 100.

Matumizi ya dawa za kulevya yanaathari mbalimbali kwa mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla. Baadhi ya madhara hayo ni kuathirika kwa afya ya mwili, matatizo ya akili na kisaikolojia, uharibifu wa mahusiano ya kifamilia na kijamii, utegemezi wa dawa hizo, kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi, kujiingiza kwenye uhalifu, na kupoteza ajira au kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Pia kuna madhara ya kiuchumi na kijamii kama vile umasikini, ongezeko la gharama za matibabu, kupoteza muda wa uzalishaji, kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kisheria au kitabibu, na kuzorota kwa maadili katika jamii. Madhara haya yote yanatoa picha ya athari kubwa zinazotokana na matumizi ya dawa za kulevya katika nyanja mbalimbali za maisha.

Mafunzo hayo yaliambatana na mada mbalimbali, ambapo mada kuu ilikuwa ni kuhusu dawa za kulevya, huku nyingine zikihusu maadili kwa watumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na kuhamasisha kilimo mbadala kama njia ya kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.






Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO