MFUMO MPYA WA KUHAKIKI SIMU WAONGEZA UFANISI WA TCRA
SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza mafanikio ya kuboresha mfumo wa kuhakiki simu za ndani na kimataifa, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa takwimu sahihi za mawasiliano nchini.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, MheJerry Silaa alisema mfumo huo umewezesha kupata taarifa za mawasiliano kwa kila mtoa huduma kwa ngazi ya mkoa na wilaya, jambo linaloimarisha ufuatiliaji na uwazi katika sekta hiyo.
"Hadi Aprili 2025, tumerekodi dakika 106,190,276 za simu za kimataifa zilizoingia nchini, ongezeko kutoka wastani wa dakika 10,968,165 Julai 2024 hadi 12,907,451 Aprili 2025," alisema Waziri Silaa.
Kwa upande wa simu za kimataifa zinazopigwa kutoka Tanzania kwenda mataifa mengine, jumla ya dakika 374,964,074 ziliripotiwa, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka dakika 28,349,598 hadi 42,195,680 kwa kipindi hicho.
Vilevile, Waziri Silaa alieleza kuwa simu za ndani ya mtandao mmoja (on-net) zilifikia dakika 62.3 bilioni, ingawa kulikuwa na upungufu kutoka dakika 7.19 bilioni Julai 2024 hadi 7.01 bilioni Aprili 2025. Simu kati ya mitandao tofauti (off-net) ziliongezeka hadi dakika 61.8 bilioni.
Akizungumzia usalama wa mawasiliano, Waziri Silaa alisema Serikali inaendelea kusimamia Kanzidata ya namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano (CEIR) ili kubaini na kuzima vifaa bandia, vilivyoibiwa au kutumika kwa njia za udanganyifu.
"Hatua hizi zinaimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za mawasiliano, pamoja na kupunguza uhalifu mtandaoni na matumizi mabaya ya teknolojia," alisisitiza Waziri Silaa.
Comments
Post a Comment