KAMISHNA KUJI AWAPONGEZA MAAFISA NA ASKARI WA UDZUNGWA KWA KUBORESHA UHIFADHI WA BIOANUWAI NA SAYANSI YA WANYAMAPORI - UDZUNGWA


Na Philipo Hassan/ Mang’ula, Udzungwa

Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, leo Julai 01, 2025 amewapongeza Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa kwa kuboresha na kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai na sayansi ya uhifadhi wa wanyamapori. Kamishna Kuji aliyasema hayo katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Hifadhi hiyo, yaliyopo katika mji mdogo wa Mang’ula mkoani Morogoro.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Kuji aliipongeza Menejimenti ya Hifadhi kwa mafanikio makubwa katika kuboresha shughuli za sayansi ya uhifadhi, hasa ikizingatiwa kuwa Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa ni moja ya maeneo ya kipekee yenye viumbehai adimu wasiopatikana mahali popote duniani.

“Nawapongeza sana kwa kulinda na kusimamia hifadhi. Mafanikio haya ni dhahiri kuwa hifadhi imeimarika katika kusimamia shughuli za sayansi ya uhifadhi ambayo ni pamoja na ufuatiliaji wa mifumo ya kiikolojia, afya za wanyamapori na kudhibiti milipuko ya magonjwa, udhibiti wa mioto, kuratibu na kushiriki tafiti mbalimbali, ufuatiliaji wa wanyama adimu, pamoja na tathmini za athari za mazingira kwa kila mradi wa maendeleo unaofanyika hapa,” alisema Kamishna Kuji.


Sambamba na hayo, Kamishna Kuji alibainisha kuwa kukamilika kwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika hifadhi hiyo kutachochea ongezeko la watalii na kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi - John Nyamhanga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Mashariki, alielezea maendeleo mbalimbali ya hifadhi kwa kugusia maeneo ya uhifadhi, utalii, miundombinu, pamoja na shughuli za ujirani mwema ambazo zinaendelea kuwa chachu ya mafanikio na maendeleo ya hifadhi hiyo.

“Afande Kamishna, Udzungwa tunaendelea kuhifadhi na kuendeleza jitihada za kushirikisha jamii katika uhifadhi kupitia miradi ya ujirani mwema jambo ambalo linasaidia kupunguza athari za ujangili na kusaidia jamii kushiriki katika kulinda hifadhi,” alisema Kamishna Nyamhanga.


Akiwasilisha taarifa ya hifadhi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Theodora Batiho - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa, alieleza mikakati mbalimbali inayotarajiwa kutekelezwa ili kufanikisha malengo ya kuongeza idadi ya watalii na mapato ya hifadhi hiyo.

“Tunatarajia kuanzisha mazao mapya ya utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni pamoja na kufungua lango la kupokea wageni eneo la Msosa na Mbatwa, kuanzisha utalii wa kuendesha baiskeli, kijiji cha utalii, zao la utalii wa michezo na matukio, pamoja na kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hifadhini,” alifafanua Kamishna Batiho.

Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa ni miongoni mwa Hifadhi za Tanzania zilizotajwa kuwania tuzo za kimataifa za World Travel Awards mwaka 2025 katika kipengele cha “Hifadhi Bora ya Milima Barani Afrika”. Kutajwa huku kunadhihirisha mchango mkubwa wa hifadhi hiyo katika uhifadhi wa viumbe hai, maendeleo ya utalii wa kiikolojia, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii kimataifa.




 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO