*KAMISHNA KUJI: “ENDELEENI KULILINDA BONDE LA USANGU KWA UHAI WA MTO RUAHA MKUU NA IKOLOJIA YA RUAHA”*
Na. Jacob Kasiri - Mbarali.
Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA CPA (T) Musa Nassoro Kuji amewataka Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Ruaha waliopo upande wa Ihefu Mashariki na Magharibi kuendelea kulilinda Bonde la Usangu linalokusanya maji kuelekea Ardhi Oevu ya Ihefu ambayo ni chanzo cha Mto Ruaha Mkuu ambao zaidi ya asilimia 60 ya maji yake yameendelea kuwa lulu kwa uhai wa mimea na wanyamapori ndani ya hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini Tanzania.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 02, 2025 katika Ofisi za Makao ya Kanda ya Kusini yaliyopo Rujewa katika Wilaya ya Mbarali alipofanya kikao kazi na makamanda wa Jeshi hilo la Uhifadhi wa vituo vya doria vya Ikoga, Tagawano, Magda, Ulanga, Kiwale na Ukwaheri.
Aidha, Kamishna Kuji aliongeza, “Licha ya kuhifadhi na kulinda maliasili hizi katika maeneo yetu ndani ya Hifadhi za Taifa 21 kwa weledi na ufanisi mkubwa, pia tutambue kuwa usalama wa nchi unatutegemea sana kwani maeneo yetu mengine yanapakana na nchi jirani hivyo tuendelee kuwa macho kuhakikisha hifadhi zetu haziwi mapango na vichaka vya kujifichia watu wasiotutakia amani.”
Vile vile, Kamishna Kuji aliwasilisha salamu kutoka kwa Bodi ya Wadhamini - TANAPA kuwa wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na Maafisa na Askari kwani mmeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali hizo.
Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meing’ataki - Mkuu wa Kanda ya Kusini, akimkaribisha Kamishna huyo alisema, “Nikupongeze kwa mafanikio makubwa kama Mkuu wetu wa Taasisi kwa tuzo saba (7) tulizoshinda, kati ya hizo mbili zimekuja kwa mara ya kwanza katika Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyonyakua tuzo ya Hifadhi Bora kwa Utalii wa Kitamaduni barani Afrika na Hifadhi ya Taifa Kitulo ikitutoa kimasomaso kwa kuwa eneo bora kwa fungate barani Afrika.”
Akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Muhsin Mchau ambaye ni Mkuu wa Vituo vya doria vya Ikoga, Tagawano na Magda alisema kuwa kama kiongozi anayewaongoza askari na baadhi ya maafisa, wanaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kulinda maliasili hizi kwa faida ya TANAPA na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhifadhi Mchau aliongeza kuwa licha ya bonde hili kukabiliwa na changamoto ya ujangili pia wameendelea kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa jamii, kudhibiti ujangili na kushughulikia migogoro baina ya binadamu na wanyamapori kwa wakati na kwa ufanisi.
Ziara hii ya kikazi ya Kamishna Kuji ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Hifadhi za Taifa 21 kwa lengo la kutoa maelekezo ya kiutendaji, kufuatilia shughuli za uhifadhi, utalii, fursa za uwekezaji na kuimarisha utendaji ndani ya shirika.
Comments
Post a Comment