BARAZA LA WAZEE MOROGORO LAFURAHISHWA NA UWEKEZAJI MKUBWA KITUO CHA KUFUA UMEME JNHPP*
📍*Wasema hali ya umeme kwa sasa Mkoani Morogoro ni shwari*
📍*Waishukuru TANESCO kwa kuwapa nafasi kutembelea Kituo hicho*
Baraza la Wazee Mkoa wa Morogoro limefurahishwa na uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia TANESCO katika kituo cha kufua umeme cha Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), baada ya kutembelea kituo hicho kama wazee wa miongoni mwa mikoa ya jirani inayopakana na kituo hicho kikubwa cha kufua umeme.
Hayo yamebainishwa na wajumbe wa Baraza hilo Septemba 10, 2025 walipotembelea kituo hicho ikiwa ni moja ya mikakati ya kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya umeme.
Mmoja wa wazee hao Silver Samweli kutoka Ifakara amesema Mkoa wao umeendelea kunufaika na uwepo wa kituo hicho.
“Faida kubwa tunayoipata kupitia Kituo hichi ni pamoja na kupata umeme wa kutosha. Awali tulikuwa na umeme unakatika katika mara nyingi sana lakini sasa hivi hali hiyo haipo tena kutokana na uwepo wa Kituo cha Mwalimu Nyerere,” amesema Samweli
Nae Tatu mbonde amesema kwa uwekezaji mkubwa aliouona katika Kituo hicho kilichobaki ni Watanzania kuwa walinzi wakuu ili kuhakikisha umeme unaendelea kuzalishwa.
“Ninawaomba wananchi wetu kiujumla pamoja na wanamorogoro, tuulinde Mradi huu kwa asilimia 100, tusiharibu vyanzo vya maji, tusilime katika vyanzo vya maji kwa sababu mito yetu ndiyo inayojaza Bwawa la Mwalimu Nyerere linalotufanya sisi tupate umeme wa uhakika,” amesema Mbonde
Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Kituo cha Bwawa la Julius Nyerere Mhandisi Manfred Mbyalu amesema miongoni wa wanufaika wa ajira wakati wa ujenzi wa Mradi wa Julius Nyerere ni pamoja na wananchi wa Mkoa jirani wa Morogoro hivyo ujio wa wazee wa Mkoa huo umekua kama ushuhuda wa kazi iliyofanyika.
“Wazee wamekuja kujiridhisha na kile kilichofanyika na kuona kweli vijana wao wameshiriki kwenye mradi huu mkubwa wa kimkakati kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi yao,” ameongeza Mha. Mbyalu
Comments
Post a Comment