DC SAME AWAWAKIA WACHIMBAJI WA MADINI WANAOACHA MASHIMO, ATAKA YAFUKIWE ILI UWEPO USALAMA WA WANANCHI NA MAZINGIRA.
DC SAME AWAWAKIA WACHIMBAJI WA MADINI WANAOACHA MASHIMO, ATAKA YAFUKIWE ILI UWEPO USALAMA WA WANANCHI NA MAZINGIRA.
Na Christina Thomas,
Same, Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, amewaagiza wachimbaji wa madini ya viwandani kuhakikisha wanafukia mashimo yanayosalia baada ya shughuli za uchimbaji, ili kuepusha uharibifu wa mazingira ikiwemo mmomonyoko wa ardhi, hali inayohatarisha usalama wa wakazi wa maeneo husika.
Agizo hilo limetolewa jana wakati wa mkutano wa wadau wa madini ya viwandani (hasa Jasi, Pozolana na Bauxite) wa Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika wilayani Same. Mheshimiwa Kasilda alisema ni lazima wachimbaji wote waliowahi kuendesha shughuli za uchimbaji na kuacha mashimo, kuhakikisha wanayafukia ili maeneo hayo yaweze kutumika kwa shughuli nyingine za kijamii au kiuchumi.
“Kuna maeneo mengi ambapo wachimbaji wameacha mashimo wazi baada ya kumaliza shughuli zao. Naagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwatafuta wachimbaji hao na kuwahimiza kuyafukia mashimo hayo kwa sababu yanahatarisha usalama wa wananchi na kusababisha uharibifu wa mazingira,” alisema.
Aidha, Mheshimiwa Kasilda aliwakumbusha wachimbaji wote wa madini kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji mara tu baada ya kupewa leseni. Alisisitiza umuhimu wa kujitambulisha kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri, Kata na kijiji husika kabla ya kuanza shughuli ili kuhakikisha usalama wa eneo, hasa kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, alisema lengo la mkutano huo ni kuweka maazimio ya pamoja katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini ya viwandani. Alibainisha kuwa mkoani humo kuna zaidi ya wachimbaji 900 wenye leseni, zaidi ya watu 100 wana leseni za utafiti wa madini, na wengine 40 wana leseni za biashara ya madini.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wa madini ya viwandani wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Emmanuel Bwambo, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wachimbaji mkoani humo, alisema sababu kubwa ya kushindwa kufukia mashimo ni bei duni ya madini hayo sokoni ikilinganishwa na gharama kubwa za uchimbaji na ufukiaji, hali inayosababisha hasara kwa wawekezaji.
Katika mkutano huo, wadau walikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kuweka bei elekezi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wanunuzi kutoka viwandani ili kusaidia kufidia gharama za ufukiaji wa mashimo.
Pia walipendekeza kufanyika kwa vikao vya pamoja kati ya wadau wa sekta ya madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Halmashauri ili kutafuta njia rafiki ya utozaji ushuru na tozo mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha kila mdau anafaidika.
Comments
Post a Comment