MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWENI MSTARI WA MBELE KUCHOCHEA MAENDELEO: DKT. BITEKO
MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWENI MSTARI WA MBELE KUCHOCHEA MAENDELEO: DKT. BITEKO
Na Musa Mathias, Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa mstari wa mbele katika kuchochea vipaumbele vya maendeleo kupitia taaluma zao katika maeneo yao ya kazi.
Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) Mei 07, 2025.
"Furukuteni kwa wote walioko juu yenu na chini yenu ili waelewe kuwa taaluma yenu ni muhimu na msingi kwa maendeleo ya Jamii hivyo msikubali kukaa nje ya ukumbi wakati mipango ya maendeleo inapangwa katika halmashauri zenu" ameeleza Dkt. Biteko.
Aidha Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inautambua mchango mkubwa wa taaluma ya Maendeleo ya Jamii hivyo ametoa wito kwa Taasisi zote kuwashirikisha wataalam wa Maendeleo katika mipango yote ya Maendeleo kuanzia awali.
“Naomba muendelee na jukumu lenu la kuwahamasisha wananchi kutambua na kuchangamkia fursa zilizomo kwenye jamii ikiwemo mikopo inayotolewa ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuletea maendeleo katika jamii” alisisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima awali akimkaribisha mgeni rasmi amewataka wataalam hao wa Maendeleo ya Jamii kuwa mabalozi wazuri wa shughuli za maendeleo zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa wananchi wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"Ninyi ni mainjinia wa mafanikio ya Jamii, nawapongeza sana kwa kuitumia taaluma yenu kuwa chachu ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, mkawe mashahidi wazuri kwa wananchi tunapoenda kwenye uchaguzi mwezi Oktoba" ameeleza Waziri Dkt. Gwajima.
Naye Rais wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Victor Kabuje akitoa salam za Chama hicho ameishukuru Serikali kwa kuajiri Wataalam wa Maendeleo ambao wamekuwa chachu ya kurahisisha uwajibikaji na kuwafikia wananchi kuanzia ngazi ya Kata.
Mkutano huo umengozwa na Kaulimbiu isemayo: "Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwa Maendeleo Endelevu na Jumuishi: Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025"
MWISHO
Comments
Post a Comment