MAFANIKIO YA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 4 YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Dar es Salaam - 15 Mei, 2025.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ya mwaka 2008, ambayo ilianza kutekelezwa rasmi mnamo tarehe 01 Julai 2015. Mfuko huu unatoa ulinzi wa kijamii kwa wafanyakazi wote walioko katika sekta ya umma na binafsi dhidi ya madhara yanayotokana na ajali, magonjwa au vifo vinavyotokea kazini au kutokana na kazi.

Kupitia WCF, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga mfumo madhubuti wa kitaasisi unaolenga kutoa huduma za fidia kwa wakati, kwa uwazi na kwa kuzingatia haki za wafanyakazi. Katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, WCF imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutimiza majukumu yake. Mafanikio haya yanaakisi utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa Sura ya 4 Ibara ya  5 juu ya maisha bora na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inaelekeza Kuimarisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili iendelee Kutoa Huduma Bora na Endelevu na kuimarisha ulinzi na ustawi wa nguvu kazi ya Taifa.

Mafanikio haya ni pamoja na:

Kushushwa kwa ada ya uchangiaji:

Serikali ya Awamu ya Sita ilitangaza rasmi kushusha Ada za uchangiaji katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 ya mapato ya kila mwezi ya wafanyakazi wao. Uamuzi huu umefanya taasisi binafsi kuchangia sawa na taasisi za Umma. Lengo ni kumpunguzia mzigo mwajiri ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia sasa azielekeze kwenye maeneo mengine ya uendeshaji na uzalishaji. 

Kutoa Msamaha wa malipo ya Riba kwa Waajiri Waliochelewesha Michango

Moja ya dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kufungua milango la kiuwekezaji na kufungua mikwamo ya biashara. Katika utekelezaji wa maono haya WCF ilifanya uchambuzi katika majukumu yake ya msingi ili kuweza kubaini vikwazo mojawapo vya kibiashara nchini na kuchukua hatua stahiki. Kuanzia Septemba, 2021 SERIKALI ilishusha Riba  kwa michango iliyocheleweshwa na waajiri kutoka asilimia 10 hadi 2 kwa mwezi kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba 2017 hadi tarehe 31 Agosti 2021. 

Kuongezeka kwa kima cha chini cha fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

Chini ya Serikali ya Awamu ya Sita - Kima cha chini cha fidia kimeongezeka kutoka utaratibu wa awali ambao haukuwa na kima cha chini cha fidia kwa mfanyakazi ambaye hakupata ulemavu wa asilimia 100 hadi kufikia shilingi 275,702.83 kwa sasa. 

Utoaji wa Fidia kwa Walengwa:

WCF imefanikiwa kuwalipa fidia wafanyakazi na wategemezi wao wapatao 19,650 waliopata ajali, ugonjwa au kufariki kutokana na kazi. Hili ni hitaji la msingi la uanzishwaji wa WCF na linaonesha utendaji wa moja kwa moja wenye tija kwa jamii ya wafanyakazi.

Upanuzi wa Mafao:

Idadi ya mafao imeongezeka hadi kufikia mafao saba makuu ambayo ni pamoja na:

Fao la Matibabu (bila kikomo)

Fao la Ulemavu wa Muda Mfupi

Fao la Ulemavu wa Kudumu

Fao la Pensheni kwa Wategemezi

Fao la Wasaidizi wa Mgonjwa

Fao la Utengamao

Fao la Msaada wa Mazishi

Uboreshaji wa Mifumo ya TEHAMA:

WCF imetekeleza mapinduzi ya kidigitali ambapo zaidi ya 90% ya huduma zote sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao. Mifumo hii imepunguza urasimu, kuongeza uwazi, na kuboresha ufanisi wa utendaji kazi.

Tuzo na Ithibati za Kimataifa:

Kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa na WCF imepelekea Mfuko kupewa Cheti cha Ithibati katika utoaji wa huduma bora kwa viwango vya Kimataifa (ISO Certification) mwezi Juni, 2024. Hatua hii inaongeza imani chanya kwa wadau wote wanaohusika kwenye mnyororo wa fidia kwa wafanyakazi nchini juu ya Taasisi hii. 

Kwenye TEHAMA, mwaka huu wa 2025 WCF wamekuwa washindi wa pili katika Tuzo zinazotolewa na Serikali Mtandao (eGA) katika Taasisi zinazoongoza katika kufuta Sheria, Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao. vilevile, TEHAMA Awards 2025, WCF wameshinda nafasi ya tatu katika taasisi za Umma nchi zinazotumia TEHAMA kuondoa Urasimu wa Utoaji Huduma. Vilevile, mwaka 2023 WCF ilishinda tuzo ya Shirikisho la Kimataifa la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (yaani ISSA) kama taasisi ya mfano katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA. Mwaka 2025, WCF ilishika nafasi ya pili katika eGA Awards na nafasi ya tatu kwenye TEHAMA Awards 2025 kwa taasisi za umma zilizofanikiwa kuondoa urasimu kupitia TEHAMA.

Utoaji wa Elimu na Uhamasishaji:

Mfuko umeendesha kampeni mbalimbali za elimu na uhamasishaji kwa waajiri na wafanyakazi juu ya haki zao, taratibu za fidia na usalama mahali pa kazi. Elimu hii imesaidia kupunguza ajali na magonjwa kazini, pamoja na kuongeza usajili wa waajiri.

Pamoja na mafanikio haya, zipo changamoto chache tunazoendelea kuzifanyia kazi. Kati ya hizo ni:

Waajiri Kutojisajili na Kutowasilisha Michango kwa Wakati: Baadhi ya waajiri bado hawajatekeleza matakwa ya sheria ya kuwasajili wafanyakazi na kuwasilisha michango kila mwezi. Hili linawanyima haki wafanyakazi wanapopatwa na majanga kazini.

 

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umejidhihirisha kuwa chombo muhimu chaulinzi wa kijamii kwa wafanyakazi nchini. Tunaahidi kuendelea kuboresha huduma, kushirikiana na wadau wote, na kuhakikisha tunasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ili kila mfanyakazi anapopatwa na madhila, anapata haki yake kwa wakati.

natoa wito kwa waajiri wote kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, na kwa wafanyakazi, kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wakijua kuwa mfuko wao uko imara na thabiti kuwahudumia.

Imetolewa na:

Kitengo cha Uhusiano kwa Umma

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)



 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO