MSIACHE KUTENDA HAKI, JAMII SALAMA INAWATEGEMEA: BI. FELISTER MDEMU

MSIACHE KUTENDA HAKI, JAMII SALAMA INAWATEGEMEA – NAIBU KATIBU MKUU MDEMU

Na Mwandishi Wetu, 

Tabora.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amewataka waratibu wa Madawati ya Jinsia katika maeneo ya umma kuwajibika na kutenda haki ili kujenga jamii salama isiyo na vitendo vya ukatili.

Bi. Felister ameyasema hayo tarehe 12 Juni 2025 wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo kwa waratibu wa madawati ya jinsia katika maeneo ya umma mkoani Tabora. Mafunzo hayo yamewaleta pamoja washiriki kutoka mikoa ya Tabora, Songwe na Rukwa.

"Matukio haya ya ukatili tutayaondoa ikiwa wote tutazungumza sauti moja, hivyo nawasihi tukatende haki, kila mmoja aone jukumu la kupinga vitendo vya ukatili ni lake," amesisitiza Naibu Katibu Mkuu Felister.

Ameongeza kuwa jamii inapaswa kufahamu na kufikisha taarifa za ukatili wa kijinsia kwa maofisa wa madawati waliopo kwenye vituo vya Polisi, vituo vya mabasi pamoja na maofisa ustawi wa jamii walioko katika halmashauri na ofisi za kata.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kujitokeza kila mara kushughulikia changamoto zinazotokana na vitendo vya ukatili.

"Sote ni mashahidi wazuri kwa hii Wizara, kila tunapowafikia kwa changamoto yeyote wamekuwa na muitikio wa haraka na tunafanikiwa kutatua changamoto hiyo bila kuwekewa vikwazo vya ucheleweshwaji," ameeleza Dkt. John.

Aidha, amesisitiza kuwa wanaume wasione haya kutumia madawati hayo katika kutoa taarifa za ukatili, kwani sasa huduma hizo zinapatikana hadi kwenye maeneo ya umma.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Rennie Gondwe, akitoa salamu za Wizara, amesema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na ukatili ndani ya jamii, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia katika maeneo mbalimbali nchini.


Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Jinsia imepanua wigo wa huduma hizo kwa kuanzisha jumla ya madawati 238 katika masoko ndani ya mikoa 19 ambayo tayari yanafanya kazi. Mafunzo mbalimbali ya namna bora ya uendeshaji wa madawati hayo yameendelea kutolewa mara kwa mara, kwa lengo la kuhakikisha jamii inaungana kwa sauti moja kukemea, kupinga na kutotenda vitendo vya ukatili.









Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO