WAKILI MPANJU ATAKA MIKAKATI KUPAMBANA NA MILA NA DESTURI ZENYE MADHARA KWA JAMII.
WAKILI MPANJU ATAKA MIKAKATI KUPAMBANA NA MILA NA DESTURI KANDAMIZI KWA JAMII.
Na Mwandishi Wetu.
Ikungi - Singida
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju ameitaka jamii kushirikiana kwa pamoja ili kubaini na kuweka misingi imara ya kupambana na Mila na desturi zenye madhara kwa jamii na ambazo zimekuwa kikwazo cha maendeleo kwenye familia na Taifa kwa ujumla.
Wakili Mpanju ameyasema hayo Juni 2, 2025 katika Kata ya Ighombwe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida wakati akizindua kitini cha wawezeshaji cha majadiliano ya mila na desturi katika jamii.
Wakili Mpanju amesisitiza kuwa jamii inatakiwa kudumisha mila na desturi nzuri zinazochangia ustawi wa Taifa ili kujenga jamii imara.
"Tumekuja kusema na wananchi tukiamini maadili, mila na desturi chanya hurithisha kizazi kimoja hadi kingine hivyo niwaombe viongozi wa dini, wazee wa Mila na jamii kwa ujumla tushirikiane na Serikali kudumisha mila chanya na vile vikwazo vya maendeleo ambavyo vinachangiwa na mila na desturi hasi tunapaswa kuvikataa" ameeleza Wakili Mpanju.
Aidha Wakili Mpanju amewashukuru wadau ambao wamekuwa wakishirikiana na Wizara ikiwemo Shirika la Amani Girls kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wanawake na wasichana pamoja na kuendeleza maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Wakili Mpanju ameongeza kwamba mila na tamaduni ni sehemu ya utambulisho wa jamii. Hivyo ni muhimu kuziendeleza zile zinazojenga mshikamano, lakini zile zinazowanyima haki watoto, wanawake au makundi mengine hazifai kuendelea katika jamii.
Amesema jamii inapaswa kuweka Mikakati ya kuhakikisha inaondokana na mila na desturi zenye madhara kwani zinapelekea uwepo wa vitendo vya ukatili katika jamii hivyo ni muhimu kupaza sauti na kutoa taarifa hasa na vitendo hivyo zinapotokea ili zifanyiwe kazi na mamlaka husika.
Akizungumza awali Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema kuwa uzinduzi huo ni muhimu sana katika kuhakikisha Kampeni ya mageuzi ya kifikra kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo ngazi ya msingi inafanikiwa kuwafikia wananchi na kubadili fikra zao katika kujiletea maendeleo.
Ameongezea kuwa wanaamini baada ya kampeni hiyo wanaighombwe watashirikiana kupanga, kumiliki, kuindeleza na kuitunza miradi yote ya maendeleo watakayoianzisha na itakayoanzishwa na Serikali katika jamii yao.
MWISHO
Comments
Post a Comment