MBUNGE MWAKIOJA AWASISITIZA WANANCHI KUENDELEA KUIAMINI SERIKALI



Na Agnes Mambo,Mkinga

Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Mhe. Twaha Said Mwakioja, amewahakikishia wananchi wa Kata ya Mwakijembe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kusimamia haki na ustawi wa kila mmoja, huku akiomba wananchi waendelee kuwa na imani na serikali wakati taratibu za kutatua changamoto zao zikiendelea kufanyiwa kazi.

Mwakioja alitoa kauli hiyo Desemba 04, 2025 wakati akishiriki hafla ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, ya kukabidhi hundi za fidia kwa wananchi waliohamishwa kupisha Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi katika Kijiji cha Mkota, Kata ya Mwakijembe, Wilaya ya Mkinga.

Mbunge huyo alibainisha kuwa changamoto za wananchi ni mchakato unaohitaji ushirikiano wa pande zote, na akatoa ahadi ya kufanya ziara kijiji kwa kijiji ili kusikiliza kero na kuzifikisha katika mamlaka husika kwa utatuzi wa haraka.


Aidha, Mwakioja alitumia nafasi hiyo kuwasilisha maombi mawili muhimu kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya wananchi:

Kwanza, kuwatupia jicho la huruma wananchi 25 ambao hawajapata stahiki zao za fidia kutokana na changamoto za kinyaraka.

“Nafahamu Mhe. RC ni mtu mwenye huruma na anayetekeleza maelekezo ya Rais wetu. Naomba wananchi hawa 25 wapewe kipaumbele ili nao wapate haki yao. Tumeona hata watumishi waliowahi kuachishwa kutokana na vyeti feki walilipwa stahiki zao kwa maelekezo ya huruma ya Mhe. Rais. Naamini na hili litawezekana,” alisisitiza.

Pili, aliiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa karibu eneo jipya walilopelekwa wananchi hao ili kuhakikisha lina miundombinu ya msingi ikiwemo maji, barabara na mazingira rafiki kwa makazi.

“Tuelekeze nguvu kuhakikisha eneo hili si tengefu tu kwa jina, bali ni mahali panapoweza kuwawezesha wananchi kuishi kwa furaha, amani na tabasamu usoni,” alisema.


Katika hatua nyingine Mhe. Mwakioja aliwashukuru Wananchi kwa namna walivyotekeleza vyema zoezi la uchaguzi mkuu uliopita na kuonesha imani kubwa kwa Serikali kwa kumpa kura nyingi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; Mbunge wa Jimbo hilo; na Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Mzee Mwadika.

“Nawashukuru sana ndugu zangu wa Mwakijembe. Pamoja na changamoto zenu nyingi, mmeendelea kuiamini Serikali yetu. Mmetupa kura za kishindo na kutuonesha dhamira yenu ya kutuunga mkono. Tutaendelea kuwa nanyi na kusikiliza kero zenu,” alisema.

Aidha alimuomba Mkuu wa Mkoa kutoa nafasi fupi kwa Diwani wa Kata hiyo, Mzee Mwadika, ili kuwahutubia wananchi wake kama ishara ya umoja na mshikamano katika hatua za kutatua changamoto zilizopo.

Tukio hilo limeacha matumaini makubwa kwa wananchi wa Mwakijembe, huku Serikali ikisisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayeachwa nyuma katika kuhakikisha haki, fidia halali na ustawi wa jamii unaimarishwa.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO