MUWSA INAVYOTEKELEZA MIRADI YA MAJI 2025/26.
MUWSA INAVYOTEKELEZA MIRADI YA MAJI 2025/26.
Na Musa Mathias.
Moshi- Kilimanjaro.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo imepanga kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 5.8 kwa ajili ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi hiyo.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 4.2 zinatarajiwa kukusanywa kutoka mapato ya ndani ya mamlaka, huku zaidi ya Shilingi bilioni 1.6 zikitolewa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji. Mgawanyo huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maji safi na maji taka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Moshi.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe, alisema kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, mamlaka imejipanga kutekeleza miradi ya kuboresha upatikanaji wa maji safi katika kata za Mweka, Sungu na Longuo A.
Alieleza kuwa miradi mingine ni utekelezaji wa miradi ya maji katika kata 12, ukarabati wa kilomita 34.5 za mtandao wa zamani wa maji, pamoja na ujenzi wa mtandao mpya wa maji safi wenye urefu wa zaidi ya kilomita 105 katika eneo lote la huduma la MUWSA.
Aidha, miradi hiyo inajumuisha kuendeleza vyanzo vya maji vya Saika na Chekereni Weruweru, ujenzi wa chujio la maji Mang’ana, ujenzi wa chemba 500 za kudhibiti upotevu wa maji, ujenzi wa mtandao mpya wa maji taka wenye urefu wa zaidi ya kilomita 10, pamoja na kuendeleza chanzo cha maji cha Njoro ya Dhobi.
Mhandisi Kija Limbe aliongeza kuwa MUWSA imebuni pia mradi wa kuendeleza chanzo cha maji cha Materuni, ambapo utekelezaji wake unategemea upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa mamlaka itaendelea kutenga fedha kutoka mapato yake ya ndani kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na majitaka katika Manispaa ya Moshi.
Akihitimisha kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwataka watendaji na viongozi mkoani humo kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na za wazi kuhusu fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema uwazi huo ni muhimu ili wananchi waweze kutambua miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kufuatilia maendeleo yake kwa karibu.
Hadi kufikia Septemba 2025, katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, MUWSA imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa mtandao wa maji safi na majitaka kwa viwango tofauti kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mradi wa ujenzi wa mtandao wa maji safi katika kata 12 umefikia asilimia 34 ya utekelezaji, ukiwa na gharama ya Shilingi bilioni 6.88, ambapo Shilingi milioni 28.16 zimetumika hadi sasa kutoka MUWSA kwa ajili ya huduma za kitaalamu.
Aidha, mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji cha Njoro ya Dhobi bado haujaanza kutekelezwa na hivyo kubaki katika asilimia 0 ya utekelezaji.
Kwa upande mwingine, mamlaka imefanikiwa kukamilisha kwa asilimia 100 mradi wa ujenzi wa mtandao wa majitaka unaounganisha Kiwanda cha Kuchakata Bidhaa za Ngozi cha Karanga–Kilimanjaro, baada ya kutumia Shilingi bilioni 1.80 zilizotolewa na Wizara ya Maji pamoja na mkopo.
Vilevile, mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji safi katika kata za Mweka, Sungu na Longuo A umefikia asilimia 33 ya utekelezaji, ambapo Shilingi milioni 540.79 zimetumika kupitia mkopo.





Comments
Post a Comment