KAMISHNA TIRA AIPONGEZA BUMACO INSURANCE KWA UFANISI MKUBWA IKITIMIZA MIAKA 45
KAMISHNA TIRA AIPONGEZA BUMACO INSURANCE KWA UFANISI MKUBWA IKITIMIZA MIAKA 45.
Na Mwandishi wetu,
Moshi, Kilimanjaro.
Wakati kampuni ya Bima ya Bumaco Insurance limited, ikitimiza miaka 45 tangu kuanzishwa kwake, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini(TIRA), Dk Baghayo Saqware ameipongeza kampuni hiyo kwa maendeleo makubwa akisema historia ya kampuni hiyo inatoa hamasa kubwa kwa wawekezaji wa Kitanzania nchini.
Hayo ameyasema wakati alipotembelea na kuzindua ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo la KNCU na Double road, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
"Niwapongeze Bumaco mmeanza hatua kwa hatua hadi kufikia kuwa kampuni imara ya bima, Mmehamasisha Watanzania wengi kuingia kwenye uwekezaji wa bima, na sisi kama mamlaka tutaendelea kuwalinda na kuwawezesha ili muwe kampuni inayotegemewa siyo tu Tanzania, bali Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla,” amesema Kamishna huyo.
Aidha, ameipongeza menejimenti ya kampuni hiyo kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja, akisisitiza kuwa Kanda ya Kaskazini ina fursa kubwa ya ukuaji kutokana na idadi kubwa ya wateja waliopo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bumaco Insurance, Dk Shirumisha Kwayu, amesema kampuni hiyo inaadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni miongoni mwa kampuni za bima zilizodumu na kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania katika sekta ya bima.
Amesema Bumaco Insurance imejikita katika kutoa huduma za bima za mali na bima za maisha kwa wateja mbalimbali, wakiwemo watu binafsi, familia, kaya pamoja na wafanyabiashara.
“Tupo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania kwa kutoa huduma za bima za magari, usafirishaji, biashara, bima za uaminifu, bima za maisha pamoja na bima za uwekezaji. Kama una biashara yako, Bumaco ipo tayari kulinda biashara na mali zako, pamoja na kuhakikisha familia yako iko salama,” amesema Dk Kwayu.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo imefungua ofisi mpya mjini Moshi, eneo la Karibu na barabara ya Double Road, hatua inayolenga kusogeza huduma za bima karibu zaidi na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
“Leo tumefurahi sana kupata ujio wa Kamishna wa Bima ambaye amefika kuzindua ofisi zetu mpya. Hii ni ishara ya kutambuliwa kwa mchango wa Bumaco katika sekta ya bima nchini,” amesema.
Dk Kwayu ameongeza kuwa Bumaco Insurance imekuwa ikifanya vizuri katika ulipaji wa madai ya bima, akisema zaidi ya asilimia 95 ya madai halali yamelipwa kwa wakati.
“Tumekuwa tukihakikisha kuwa madai yote yanapitia uhakiki, na pale yanapothibitika kuwa halali, tunayalipa kwa haraka na kwa uadilifu mkubwa,” amesema.
Mwisho..



Hongera saaana Dr. Shirumisha na team nzima kufikia hatua hii. Hakika Bumaco ni jibu letu kwa bima na elimu
ReplyDelete